Ubalozi wa Uswisi nchini wachangia Tamasha la Sauti za Busara

603
0
Share:

Ubalozi wa Uswisi umechangia zaidi ya shilingi milioni 260 ili kuwezesha tamasha la muziki la Sauti za Busara kwa miaka mitatu ijayo. Balozi wa Uswisi nchini Tanzania, Mhe. Florence Tinguely Mattli, alikutana na Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya Busara Promotions Mhe. Simai Mohammed kwa ajili ya makabidhiano katika ofisi za Ubalozi jijini Dar es Salaam Februari 3.

Sauti za Busara ni kati ya matamasha ya muziki yanayoheshimika sana barani Afrika. Tamasha hili la kipekee linahamasisha kuheshimu tofauti kati ya watu kwa kuleta watu pamoja kusherehekea muziki ‘live’ kutoka Barani la Afrika. Lengo la tamasha hili ni kuongeza ujulikanaji na upatikanaji kwa muziki wa Afrika, kuendeleza ujuzi na fursa kwa ajili ya wale walio katika sekta ya muziki na kuimarisha ushirikiano na mitandao ya muziki kikanda na kimataifa.

“Uswisi imekuwa ikisaidia matukio na juhudi mbalimbali katika sekta ya sanaa na utamaduni nchini Tanzania kwa zaidi ya miaka kumi sasa,” alisema Balozi Tinguely Mattli. “Tamasha la Sauti za Busara ni mfano mzuri wa tukio kitamaduni ambalo huleta watu pamoja ili kufurahia kazi za sanaa na wakati huo huo kuchangia maendeleo ya kiuchumi.”

Mheshimiwa Simai alitoa shukrani kwa niaba ya Bodi ya Wadhamini ya Busara Promotions kwa msaada huo. “Mashirika ya sanaa na utamaduni yanategemea sana ufadhili wa wadau wa maendeleo. Tunashukuru Ubalozi wa Uswisi kwa mchango wao katika kuwezeshaea kufanikisha tamasha hili,” alisema.

Tamasha la Sauti za Busara litaanza tarehe 9 na kufikia tamati tarehe 12 Februari 2017 katika ukumbi wa kihistoria wa ‘Old Fort’ mjini Stone Town.

Share:

Leave a reply