Uongozi wa mgodi wa CATA watakiwa kuzungumza na serikali ya kijiji ili kuondoa tofauti

66
0
Share:

Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo ameuagiza Mgodi wa Dhahabu wa CATA Mining uliopo katika Kijiji cha Kataryo Mkoani Mara kukaa pamoja na Serikali kujadili tofauti zilizopo ili kuruhusu mgodi huo kuendelea na shughuli za uzalishaji.

Alitoa agizo hilo Desemba 28, 2017 kwenye mkutano na wananchi katika Kata ya Tegeruka kufuatia ombi kutoka kwa mmoja wa Wakurugenzi wa mgodi huo, Mahuza Nyakirang’ani  pamoja na wananchi waliokuwa wakifanya kazi kwenye mgodi huo na wananchi wa maeneo ya jirani na mgodi waliokuwa wakinufaika na mgodi kwa namna mbalimbali la kuruhusu uzalishaji uendelee.

Alisema anatambua umuhimu wa mgodi huo kwa wamiliki na wananchi kwa ujumla na hivyo ipo haja ya kukaa pamoja kujadili tofauti zilizosababisha kusimamishwa kwa uzalishaji katika mgodi huo ili uendelee na uzalishaji.

Alisema uangaliwe uwezekano wa kuruhusu uzalishaji uendelee ili wananchi waliokuwa  wameajiriwa mgodini hapo waendelee na ajira zao huku majadiliano yakiendelea kufanyika.

“Kama mlivyonieleza kuna baadhi yenu mlikua mkifanya kazi kwenye mgodi lakini tangu mgodi usimamishwe uzalishaji nanyi hamna kazi, kwahiyo ni vyema wakati mazungumzo yanaendelea na mgodi ukawa unazalisha ili waliokosa ajira warudi kazini,” alisema.

Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Kataryo, Kata ya Tegeruka Wilaya ya Musoma Vijijini (hawapo pichani) wakati wa mkutano wake na wananchi waishio maeneo jirani na Mgodi wa Dhahabu wa CATA Mining.

Aidha, akizungumza kwa niaba ya wananchi waishio maeneo jirani na mgodi, Elizabeth Masabu ambaye ni Mjumbe wa Serikali ya Kijiji cha Kataryo alimueleza  Naibu Waziri Nyongo kuhusu uhusiano baina ya mgodi na wananchi na pia kumuomba kuingilia kati masuala mbalimbali ikiwemo ajira kwa wananchi wa maeneo husika, fidia, utunzaji wa mazingira na migogoro na mgodi.

Masabu aliongeza kuwa waliingia mikataba ya kirafiki na mgodi huo ambao alisema kuna makubaliano ambayo hayajafanyika na hivyo alimuomba Naibu Waziri kuwasaidia kuhakikisha mgodi huo unarejea makubaliano.

Akijibu hoja za wananchi hao, Nyongo aliuagiza mgodi kuhakikisha unaingia mkataba wa kisheria wa uwajibikaji kwa jamii (corporate social responsibility) ili Serikali ya Kijiji iweze kujipatia haki yake kwa mujibu wa makubaliano ya mkataba.

Aliuagiza mgodi huo kutoa kipaumbele cha ajira kwa wananchi wa maeneo ya jirani kwa kazi wanazoziweza na wakati huohuo aliwaasa wananchi watakaonufaika na ajira wafanye kazi kwa uadilifu.

Kwa upande wake Nyakirang’ani  alimuahidi Naibu Waziri Nyongo kwamba mgodi huo utaendelea kuboresha mahusiano na jamii na kwamba watatekeleza maagizo yake kwa wakati ikiwemo suala la ulipaji wa fidia.

Share:

Leave a reply