Viongozi wa dini waombwa kuwafundisha waumini faida za utunzaji mazingira

83
0
Share:

Serikali ya Mkoa wa Shinyanga na Tabora imetoa wito kwa viongozi wa dini mbalimbali kuhakikisha wanasaidia katika utoaji wa elimu kwa waumini wao juu ya umuhimu wa upandaji miti na uhifadhi wa mazingira ili kuinusuru Mikoa hiyo isijekueuka kuwa sehemu ya jangwa kutokana na ukataji ovyo wa mistu.

Wito huo umetolewa  Mkoani Tabora na Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Zainabu Telack na Mwenyeji wake Aggrey Mwanri wakati wa kongamano la siku moja la mazingira ambalo lilienda sanjari na uzinduzi wa kitalu cha miche na miti 20,000 kwenye Ofisi ya Mkoa.

Telack alisema ni vema viongozi wa dini zote kuungana kwa pamoja kuhakikisha wanatumia sehemu ya muda wa kila ibaada kuwasisitiza waumini kujenga tabia kuhifadhi mazingira na kupanda miti na kuitunza kwa ajili ya manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.

“Tunawaomba viongozi wetu wa dini zetu zote kutumia nguvu yenu katika kuwaelimisha waumini wenu juu hatari itakayotokea kama tusipotunza mazingira na kupanda miti mipya…tumie lugha ambayo itasaidia kufikisha ujumbe ili hatimaye nao washiriki kikamilifu katika upandaji miti kwa ajili ya faida ya mikoa yetu na Tanzania kwa ujumla,” alisisitiza Mkuu huyo wa Shinyanga.

Alisema pamoja na viongozi wa dini kutoa elimu pia nguvu za pamoja zinahitajika kutoka kwa viongozi ,watendaji na wananchi walioko katika mikoa ya Kanda ya Ziwa na Magharibi na Kati ili  kupambana na uharibifu unaofanyika ndani ya mistu ya hifadhi na maeneo mengine na baadhi ya watu kwa maslahi yao.

Telack alisema wapo baadhi ya watu ambao baada ya kuharibu katika maeneo yao wanahamia maeneo mengine ili kuendeleza uharibifu katika mistu ya hifadhi kwa kuanzisha kilimo au kuendesha ufugaji usio rafiki na mazingira na ndio maana ipo haja ya kuunganisha nguvu katika kukabiliana na tatizo hilo.

Vile vile Mkuu huyo wa Mkoa wa Shinyanga aliwaagiza Maafisa Uhamiaji kuwachunguza kwa makini baadhi ya watu waliomo katika mistu wakiendesha uharibifu katika mistu ya Mikoa hiyo sio raia wa Tanzania na kuongeza wakishamaliza kuharibu mistu ya hapa nchini wanarudi kwao na kuwaachia Watanzania hasara.

“Niliwahi kupitia njia hii katika Wilaya ya Kaliua ,nikasimama kununua mahindi kwenye msitu , lakini aliyekuwa niuzia alikuwa akiongea Kiswahili ambacho kinaonyesha sio Mtanzania…Uhamiaji fanyieni uchunguzi hilo…kuna wageni wako msituni wanamaliza miti yetu,” alisema Mkuu huyo wa Mkoa.

Alisema baadhi ya watu wanapoulizwa mara nyingi wamekuwa wakisingizia kuwa wanatoka Mkoa wa Kigoma lakini ongea yao inaonyesha sio raia wa Tanzania.

Kwa upande wa Mkoa wa Tabora Aggrey Mwanri alisema wameamua kuanzisha kitalu hicho cha miche 20,000 kwenye Ofisi yake ili iwe sehemu ya shamba darasa kwa ajili ya wananchi na wadau mbalimbali kwenda kijifunza juu ya maandalizi ya miche ya miti kwa ajili ya kwenda kuipanda sehemu mbalimbali.

Alisema miche hiyo itagawanywa kwa wananachi mbalimbali kwa ajili ya kuipanda katika maeneo yao kwa utaratibu wa kuwaorodhesha wale wote ambao watakuwa wamepatiwa.

Mwanri aliongeza utaratibu huo wa kuwa na vitalu utashuka hadi ngazi za chini ambapo katika kila Mkuu wa Wilaya ni lazima kuwepo na kitalu cha miche 10,000, Afisa Tarafa miche 5,000, Mtendaji Kata miche 2,500 na  Mtendaji wa Kijiji miche 1,250.

Aidha alisema ili kudhibiti uharibifu Serikali itaendelea kusimamia sheria kwa ajili ya kuhakikisha hakuna uharibifu unaofanyika ndani ya mistu ya hifadhi.

Kongamano hilo ambalo lina kauli mbiu ya Tabora na Shinyanga ya kijani inawezekana kila mtu atomize wajibu wake lilitanguliwa na maandamano ya amani kutoa kwenye mnara wa Mwalimu Nyerere hadi Ofisi ya Mkuu wa Mkoa

Na Tiganya Vincent, Tabora

Share:

Leave a reply