Viongozi wa michezo watakiwa kuboresha michezo katika maeneo yao

215
0
Share:

Viongozi wa michezo ngazi za mikoa na wilaya wamehimizwa kuhamasisha na kusimamia mchezo wa riadha na michezo mingine katika maeneo yao ili taifa liweze kuwa na wanamichezo bora.

Kauli hiyo imetolewa na Naibu Waziri wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Juliana Shonza wakati alipokuwa akifunga mshindano ya mbio za Rock City Marathoni yaliyofanyika mwishoni mwa wiki Jijini Mwanza.

“Viongozi wa michezo ngazi ya mikoa na wilaya mnawajibu wa kuhamasisha mchezo wa riadha katika maeneo yenu ili taifa liweze kuwa na wanamichezo wengi zaidi na bora nchini,” alisema Naibu Waziri Shonza.

Naibu Waziri huyo amewapongeza waandaji wa mbio hizo ambao ni kampuni ya Capital-Plus International Ltd kwa kuwa wabunifu na kufanikisha mashindano hayo kila mwaka ambapo mwaka huu yamebeba dhima ya kujenga taifa kwa kuibua vipaji vya vijana haatua ambayo inatoa fursa ya vijana hao kujiajiri kupitia mchezo wa riadha.

Mashindano ya Rock City Marathon, yamnaendelea kutoa fursa ya kutambua vipaji vya wanariadha wengi zaidi ambao kupitia mashindano hayo wanapata fursa ya kujiajiri, kuinua vipato vyao na uchumi wa taifa pamoja na kuiweka Kanda ya Ziwa katika ramani ya michezo ndani na nje ya nchi.

Aidha, kuhusu ushiriki mdogo wa Watanzania katika mashindano hayo, Naibu Waziri Shonza amewahimiza waandaaji wa mashindano hayo kuyatangaza kwani inaonekana hayajatangazwa vya kutosha ili kupata washiriki wengi wengi zaidi.

“Wakati nakimbia mbio za kilometa tatu, njiani nimewasikia wananchi wakazi wa Mwanza wakisema, kumbe kuna mashindano, ningejua ningejiandikisha kushiriki ili kufanya mazoezi,” alisema Naibu Waziri Shonza.

Kwa upande wake Rais wa Shirikisho la Riadha nchini ambaye pia na Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Bw. Athon Mtaka amesema kuwa mbio hizo ni za pili kwa ukubwa Tanzania na zinafanyika kwa mara ya nane mfululizo zikihusisha mbio za Kilometa 42, 21, 05, 03 na kilometa 2.5 ambazo zinawahusisha watoto wadogo.

“Tanzania hatuna wachezaji wengi sawa na Kenya, ili  kufuzu kushiriki mashindano ya kimataifa ni lazima mwanariadha aliyeshiriki mashindano ya kimataifa anatakiwa kukaa siku 90 za kupumzika na kuendelea kufanya mazoezi bila kushiriki mashindano mengine,” alisema Mtaka.

Bw. Mtaka alitoa ufafanuzi huo kufuatia wananchi wengi waliokuwepo uwanjani hapo kuhoji na kutaka sababu za mwanariadha Alphonce Simbu kutokuwepo katika mashindano hayo.

Katika mbio za kilometa 42 kwa wanaume wanariadha kutoka nchini Kenya ndio walitawala mbio hizo wakiongozwa na Abraham Too mshindi wa kwaza hadi nafasi ya saba ambapo nafasi ya nane ilishikwa na Mtanzania Paschal Mombo huku upande wa wanawake katika mbio hizo Wakenya wakiongozwa na Gladness Otare. 

Mshindano ya mbio za Rock City Marathoni mwaka huu yameongozwa na kaulimbiu inayobeba dhana ya kutangaza vivutio vya utalii vilivyopo katika nchi yetu “Kutangaza vivutio vya utalii kwa njia ya michezo”. Kaulimbiu hii inauunga mkono juhudi za Serikali za kufikia chumi wa kati ifikapo 2025 na kuifanya Tanzania kuwa nchi ya uchumi wa viwanda.

Na Eleuteri Mangi, WHUSM- Mwanza

Share:

Leave a reply