Wabunge wa Geita waitaka Serikali kumfuta kazi RPC wa Geita

1772
0
Share:

Wabunge wa majimbo ya Geita wameitaka serikali kupitia Wizara ya Mambo ya Ndani kufanya mabadiliko ya uongozi wa Jeshi la Polisi wilaya na Mkoa wa Geita akiwemo kamanda baada ya kulituhumu jeshi hilo kushindwa kuthibiti mauji yenye utata ya walinzi ambayo yamekuwa yakitokea mara kwa mara katika mji wa Geita.

Wabunge hao Costantine Kanyasu wa Jimbo la Geita Mjini na Joseph Kasheku Msukuma wa Jimbo la Geita Vijijini wamesema jeshi hilo badala ya kutumia mbinu za upelelezi kuthibiti mauaji hayo limekuwa likiendesha msako nyakati za jioni na usiku kupiga watu kama njia ya kumaliza matukio hayo.

Wakizungumza kwenye mkutano wa hadhara Uliofanyika kwenye uwanja wa CCM mkoa wa Geita wamesema Jeshi la Polisi wilaya na mkoa wa Geita limeshindwa kumaliza mauaji hayo ili hali yamekuwa yakitokea mjini Geita ambapo ofisi za jeshi hilo mkoa zinapatikana.

Mbunge Kanyasu amesema tatizo kubwa lililopo ndani ya Jeshi la Polisi katika mkoa wa Geita ni udhaifu kwenye kitengo chake cha upelelezi na kwamba vitisho vya polisi kwa raia sio suluhisho la mauaji hayo.

Kwa mujibu wa mwenyekiti wa Umoja wa Kampuni binafsi za Ulinzi mkoa wa Geita Ayubu Mwita ni kwamba takwimu za mauaji hayo zinaonyesha kuwa walinzi 26 wameuawa kwa nyakati tofauti kwa kipindi cha kuanzia mwaka 2014 hadi Juni 2017.

Mauaji ya walinzi katika Mji wa Geita yanadaiwa kuhusishwa na imani za kishirikina na kwamba kwa sasa jeshi hilo linaendesha msako wa kukamatwa wahusika wa mauaji hayo, ingawa msako huo umekuwa kero kwa wananchi baada ya kutishwa na wengine kushambuliwa na Askari Polisi wakiwemo wa kikosi cha kutuliza ghasia FFU nyakati za jioni na usiku.

 Na Emmanuel Twimanye, Geita

Share:

Leave a reply