“Wadau Jitokezeni kuwekeza vifaa vya kisasa katika tasnia ya filamu”– Kikwete

416
0
Share:

Wadau mbalimbali ndani na nje ya nchi wametakiwa kujitokeza na kuwekeza katika vifaa vya kisaa vya kurekodia filamu ili sekta ya filamu nchini Tanzania iweze kuendelea zaidi na kuvuka mipaka kwa kuwa na ubora wa kuweza kushindana na filamu za nchi nyingine.

Rai hiyo imetolewa na Rais Mstaafu Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete alipokua akizindua chaneli mpya ya Jason’s Televisheni itakayokuwa ikionyesha filamu mpya za kitanzania inayopatikanakatika king’amuzi cha Star times chaneli namba 126 jana Jijini Dar es Salaam.

“Wadau wa tasnia ya filamu nchini hasa waandaaji wa filamu mnapaswa kuangalia namna ya kupata wadau watakaosaidia kuwekeza vifaa vya kisasa vya kurekodia na kwa upande wangu nitajaribu kuwakutanisha na wadau wenye uwezo wa kuwekeza ili muangalie namna ya kuzungumza nao na kuwekeza vifaa vitakavyowawezesha kuandaa filamu zenye ubora na kukidhi hadhi ya kushindana kimataifa,” amesema Mhe. Kikwete.

Aidha Mhe. Kikwete amesema kuwa kuwepo kwa chaneli ya JTV itakayokua ikirusha filamu mpya za kitanzania ni jambo muhimu sana katika historia ya tasnia ya filamu hapa nchini hivyo uzinduzi wa chaneli ya JTV unafungua ukurasa mpya katika maendeleo ya tasnia ya filamu ambayo imekua ikikua kwa kasi.

Mhe. Kikwete amesema kuwa kufanikiwa kwa chaneli ya JTV kutapunguza machungu mengi ya watayarishaji wa filamu kwa kutatua changamoto ya kutokuwa na soko la uhakika na kuleta nuru ya matumaini kwa wasanii kwa kupata malipo yanayostahili kwa vipaji vyao, jasho lao pamoja na gharama wanayoingia katika kutengeneza filamu.

Kwa upande wake Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe amesema kuwa uanzishwaji wa chaneli ya JTV ni moja ya mikakati kadhaa ya kuboresha usambazaji wenye tija wa filamu mpya za kitanzania hivyo kuwataka watayarishaji wa filamu kuthamini mandhari za filamu zetu kwani filamu iliyokosa hata dakika moja kuonyesha vivutio vya utalii tulivyonavyo inakosa sifa ya ubora.

Awali Mhe. Mwakyembe amesema kuwa Tanzania itabaki kuwa chimbuko la lugha ya Kiswahili ambayo ni lugha ya 10 kuzungumzwa na watu wengi duniani kati ya lugha 6000 hivyo ni matarajio ya wizara baada ya muda mfupi mtu akisikia ala za nyimbo za Kiswahili katika filamu zetu kama vile Mdumange, Sindimba nk. ajue anaangalia filamu ya kitanzania.

Naye Kaimu Katibu Mtendaji Bodi ya Filamu Bw. Benson Mkenda amesema kuwa bodi ya filamu ipo tayari kushirikiana na wadau wote katika tasnia ya filamu wenye nia ya kukuza na kuendeleza tasnia kama ilivyo kwa Jason’s TV ambao lengo lao mahususi limelenga kuendeleza sekta ya filamu hasa katika eneo la usambazaji ili kuweza kuitoa sekta hii mahali ilipo na kuifikisha katika viwango vya kimataifa.

Na Genofeva Matemu – WHUSM

Share:

Leave a reply