Wadau wa elimu waendelea kujadili changamoto za elimu

377
0
Share:

Ikiwa ni siku ya pili ya mkutano wa wadau wa elimu nchini kujadili changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta ya elimu wajumbe wameendelea kuibua changamoto anuai huku wakiiomba Serikali kukubali sehemu ya mapendekezo hayo ili kuboresha elimu.

Miongoni mwa changamoto zilizoibuliwa na wadau hao wakati wa majadiliano ni suala la lugha ya kufundishia na tafsiri ya elimu bila ada inavyoleta mkanganyiko huku baadhi ya maeneo ikichangia jamii kujitoa katika suala zima la uboreshaji wa elimu kiujumla.

Akizungumza katika majadiliano Mwalimu Mkuu Shule ya Msingi Mkwanyule Kilwa alisema kwa kuwa mara kwa mara watafiti wengi wa elimu wameeleza kuwa kufanya vibaya kwa wanafunzi wa sekondari nchini kunachangiwa kiasi kikubwa na lugha ya kufundishia yaani kiingereza kuna haja kufanya mabadiliko ya lugha hiyo.

Alisema lugha ya kiingereza imeonekana kuwa kikwazo kwa wanafunzi kuelewa wanachofundishwa huku ikijenga matabaka kwa jamii, hasa kwa wanafunzi kutoka katika shule zinazofundishia kwa lugha hiyo tangu madarasa ya awali ‘english Medium’.

Mratibu wa Mtandao wa Elimu Tanzania (TenMeT), Bi. Cathleen Sekwao akichangia mada alisema hawashauri kiingereza kiondolewe moja kwa moja lakini kinaweza kuangaliwa pa kuwekwa na kufundishwa kama somo huku lugha ya kiswahili ikitumika kufundishia.

Alisema awali waliwai kutoa ushauri kuwa sera ya elimu itamke wazi kuwa kiswahili kitumike kufundishia kuanzia elimu ya awali hadi vyuoni lakini maoni hayo hayakuchukuliwa yalivyo na matokeo yake Sera ya elimu iliongeza kuwa Kiswahili na Kiingereza lugha zote zitumike kufundishia.

“Mimi nashauri tuimarishe lugha zote mbili ili tuweze kukubalika popote hata nje ya mipaka yetu…kama ni kiingereza basi tuanze kukiimarisha tangu darasa la kwanza ili mtoto anapofika sekondari isiwe kikwazo kwake. Suala la kuchanganya lugha zote ndio linaendelea kuleta mkanganyiko,” alisema Sekwao.

Mwalimu wa Sekondari Nanyumbu mkoani Mtwara, Mussa Mwamisori alisema baadhi ya wanafunzi wamekuwa wakitamka wazi mbele ya wazazi wao wanaacha shule kwa kuwa hawaelewi na wengine kukimbia shuleni kwa visingizio hivyo.

“Mie kwa mwaka huu pekee nimefuatwa na wanafunzi watatu wakiwa na wazazi wao wakidai wanaacha shule kwa kuwa hawaelewi, licha ya kutokubaliana nao lakini utashangaa mtoto anatoweka haji shule tena,” alisema Mwalimu Mwamisori ambaye ni mwalimu wa nidhamu.

Hata hivyo alishauri elimu zaidi itolewe kwa jamii kujua umuhimu wa elimu kwani wapo wazazi wanajiondoa katika kuchangia mafanikio ya elimu kwa kutojua umuhimu huo. Alisema mfumo wa sasa elimu bure umeleta mafanikio na changamoto, kwani wazazi wamejiondoa kabisa kuchangia hata masuala ya msingi kwenye elimu ya watoto wao ambayo Serikali haiwezi kufanya yote kwa asilimia 100.

“..Hii ni hatari sana wazazi wapo tayari kuchangia sherehe za mahafali lakini si ujenzi wa choo shuleni, ambacho ukiangalia ni suala la muhimu kwa elimu ya watoto wetu, hili limetokea kwetu,” aliongeza mwalimu huyo.

Share:

Leave a reply