Wafanyabiashara Machinga Complex kutafutiwa mikopo

575
0
Share:

Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kupitia Menejimenti ya Dar es Salaam Business Park (Machinga Complex) inatarajia kuanza utekelezaji wa mpango wa kuwajengea uwezo wa kifedha wafanyabiashara ndogondogo (Wamachinga) kwa kupata mikopo ya masharti nafuu kutoka katika taasisi za kifedha nchini.

Wakati akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, Kaimu Meneja wa Machinga Complex, Ananinas Kamundu amesema lengo la kutekeleza mpango huo ni kuwavutia wamachinga hasa wanaofanyabiashara katika sehemu zisizo rasmi kuomba nafasi za kufanya biashara katika kituo hicho.

“Menejimenti ya Machinga Complex inatoa wito kwa wafanyabiashara kutoka sehemu mbalimbali za jiji kuomba nafasi za kufanya biashara ili waweze kuingizwa katika mpango huo. Kwa kuwa huduma, miundombinu na mazingira ya biashara katika eneo hilo yameboreshwa,” amesema.

Aidha, Kamundu amesema Menejimenti yake haitasita kunyang’anya maeneo ya biashara wafanyabiashara wasiyotumia kwa muda mrefu maeneo hayo.

“Tuna wafanyabiashara wenye vizimba vyao ila wamefunga kutokana na ugumu wa biashara na kwenda sehemu zisizo rasmi , tunafanya utaratibu wa kuwakusanya na kuwashawishi ili warejee na watakao kataa kwa kipindi hicho watanyang’anywa vizimba vyao,” amesema.

Share:

Leave a reply