Waga yaiomba serikali kuingilia mgogoro wake na kijiji cha Ulata

371
0
Share:

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Hifadhi ya Wanyapori Waga, Amon Kisinga ameiomba serikali kusaidia tatizo la mgogoro wa mpaka uliopo kati ya Jumuiya  hiyo na Kijiji cha Ulata ambao unakwamisha shughuli za ulinzi wa wanyamapori kwa kuzingatia kuwa ni eneo muhimu kwa uhifadhi.

Alisema kuwa Waga ni asasi inayovutia iliyojaliwa vivutio vingi vya utalii na hii ilithibishwa zaidi na utafiti wa mambo ya wanyamapori uliofanywa na shirika la jamii la  kuhifadhi wanyamapori (WCS) mnamo mwezi Mei mwaka 2015.

Kisinga alishukuru shirika la hifadhi la WCS kwa kuwajengea ofisi ambayo itakayosaidia kuendelea kupambana na vitendo vya ujangili.

Alisema kwa WCS wamekuwa bega kwa bega katika mchakato wa uanzishwaji wa jumuiya hiyo tangu mwaka 2008, hadi kuidhinishwa kwake mwaka 2015 na kupata hati ya matumizi ya wanyamapori (user right) mwaka 2016.

Kisinga alisema kuwa WCS walisadia kuwaunganisha na taasisi zingine zinazopambana na ujangili kama vile Hifadhi ya Taifa ya Ruaha (RUNAPA) na Kikosi maalum cha kupambana na ujangili (KDU), kanda ya Iringa.

Jumuiya ya Hifadhi ya Wanyamapori Waga, ina ukubwa wa eneo  km za mraba 315 na inaundwa na jumla ya vijiji vitano ambavyo ni Nyakadete, Nyamakuyu, Igomaa, Ihanzutwa na Mahuninga, vyote vikiwa na nia ya kulinda na kusimamia rasilimali za wanyamapori kwa matumizi endelevu.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori Profesa Alexander Songorwa amewataka wananchi waishio kandokando mwa maeneo yaliyohifadhiwa kutorubuniwa na waharifu kwa kushiriki vitendo vya ujangili.

Alisema kuwa wananchi kamwe msikubali kurubuniwa na kutumika katika uharifu huo kwani kuathiri mchango wa rasilimali kwenye uchumi wa taifa, na  kuongeza kuwa kwa kufanya hivyo kunawanufaisha waharifu  wachache wakati wanajamii wakiendelea kukosa mapato na huduma za kijamii.

Profesa Songorwa aliyasema hayo wakati  akizindua jengo la ofisi ya jumuiya ya hifadhi ya wanyamapori ya Waga uliyofanyika katika Kijiji cha Nyakadete wilayani Mbarali, mkoani Mbeya jana.

“Kwa miaka ya hivi karibuni nchi yetu imeshuhudia ongezeko la ujangili na miongoni mwa sababu zinazochangia ni kukua kwa soko la meno ya tembo nje ya nchi yetu hususani mashariki ya kati na bara la asia; mmomonyoko wa maadili kwa baadhi yetu, vitendo vya rushwa vinavyosababisha wananchi wa kipato cha chini kurubuniwa na kujiingiza kwenye ujangili pamoja na ukiukaji wa sheria ya uhifadhi,” alisema Profesa Songorwa.

Alisema kuwa pamoja na ujangili kumekuwa na ongezeko la uvamizi wa maeneo yaliyohifadhiwa kwa ajili ya uchungaji mifugo, kilimo, uchimbaji madini na kuanzisha makazi.

“Haya yote huambatana na uchomaji moto na ukataji miti, vitendo vinavyosababisha uharibifu wa mazingira, ukiwemo uharibifu wa vyanzo vya maji,” alisisitiza Profesa Songorwa.

Alisema kuwa kuongezeka kwa migogoro inayosababishwa na wanyamapori wakali na waharifu huchangiwa kwa kiasi kikubwa na watu kutoheshimu mipaka kwa kuvamia maeneo yaliyohifadhiwa au kusogea kabisa  na maeneo ya wanyamapori.

Aidha, Mkurungenzi huyo wa Idara ya wanyamapori kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii alitumia nafasi kushukuru shirika lisilo ya kiserikali la WCS na  wafadhlii wao USAID kwa kuijengea Jumuiya ya Hifadhi ya Wanyamapori Waga jengo la ofisi kutakakosaidia kupunguza ujangili.

Alisema kuwa serikali kama mdau mkubwa wa uhifadhi itaendelea kujenga uelewa na kuwahamasisha wananchi na wadau wengine kushiriki uhifadhi hususan kuwaokoa wanyamapori walioko hatarini kutoweka kama vile tembo, faru, mbwa mwitu na wengineo.

Jumuiya ya Uhifadhi ya wanayamapori ya Waga (CWMA) ni moja ya Jumuiya ya Uhifadhi za wanayamapori 22 zilizopo Tanzania.

Waga inaundwana na vijiji vitano kutoka katika wilaya tatu, ambavyo ni Nyakadete na Nyamakuyu (wilaya ya Mbarali, Mbeya), Igomaa na Ihanzutwa (Wilaya ya Mufindi, Mkoa wa Iringa ) na Mahuninga (Wilaya ya Iringa, Mkoa wa Iringa).

Na Friday Simbaya, Mbarali

Share:

Leave a reply