Wahalifu 71 wakamatwa ndani ya wiki Gongo la Mboto

240
0
Share:

Jumla ya wahalifu 71 wamekamatwa ndani ya siku 7 katika maeneo mbalimbali katika Kata ya Gongo la mboto,Wilaya ya Ilala, Jijini Dar es Salaam wakiwa na kete za bangi pamoja na madumu ya pombe aina ya  gongo.

Idadi hiyo imetajwa leo Jijini Dar es salaam na Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa polisi, Bw. Lucas Mkongya alipokua akifafanua juu ya malalamiko ya wananchi wa Gongo la Mboto kuhusu uhalifu uliokithiri katika  maeneo hayo pamoja na jitihada wanazozichukua katika kuzuia uhalifu huo.

“Kweli uhalifu upo na kila siku tunajitahidi kufuatilia maeneo yote ya Gongo la Mboto. ndani ya  siku saba kuanzia Aprili 14 hadi 20 mwaka huu tumekamata jumla ya kete za bangi 640 pamoja na lita 90 za pombe aina ya gongo”alisema Kamishna Msaidizi Mkongya.

Kamishna Msaidizi Mkongya amesisitiza wananchi kushirikiana na Jeshi la Polisi kwa kutoa taarifa za wahalifu pia amewaomba wananchi wajitahidi  kuunda ulinzi shirikishi utakaosaidia kulinda maeneo yao  kwa sababu polisi pekee  hawawezi kulinda kila nyumba.

Aidha, Kamishna Msaidizi Mkongya ametoa rai kwa wazazi kutoa malezi mazuri kwa watoto wao kwa kuwa asilimia kubwa ya wezi wa maeneo hayo ni watoto wao wenyewe.

Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na walinzi shirikishi wanajitahidi kufanya doria kila siku katika maeneo mbalimbali Jijini Dar es Salaam ili kuhakikisha wahalifu wote wanakamatwa na kuchukuliwa hatua stahiki.

Imeandaliwa na Jacquiline Mrisho – MAELEZO

Share:

Leave a reply