Wajasiriamali wanawake kutoka nchini wafanya ziara Comoro

332
0
Share:

Kikundi cha wajasirimali wanawake kutoka Tanzania (Tanzania Saccos for Women Enterprenuers) kinachoongozwa na Bi. Anna Matinde Mkurugenzi wa Bodi ya Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania waliwasili nchini Comoro kwa ajili ya ziara ya siku mbili. Lengo la ziara hiyo ni kutafuta masoko kwa ajili ya bidhaa za kutoka Tanzania, pamoja na kukutana na wajasiriamali wa Comoro ili kuweza kubadilishana taarifa juu ya fursa mbalimbali za biashara kati ya Tanzania na Comoro.

Wajasirimali hao waliwasili nchini Comoro tarehe Juni, 13 na kupokelewa na  Balozi wa Tanzania nchini Comoro Mhe. Chabaka F. Kilumanga. Wakati wakiwa nchini Comoro, wajumbe walipata fursa ya kukutana na wajumbe kutoka sekta binafsi ya Komoro pamoja na wa Tanzania waishio Comoro (Diaspora). Ujumbe huo ulifurahishwa sana na fursa za biashara zilizopo Comoro ambapo walielezea kuwa wapo tayari kushirikiana na Wakomoro katika kuleta bidhaa mbalimbali katika soko la Comoro.

Aidha, wajumbe walipata fursa ya kukutana na kufanya mazungumzo na Jumuiya ya Watanzania waishio Komoro (TADICO). Katika majadiliano yao, wajumbe waliweza kushaurina juu ya mikakati ya kufanya biashara nchini Comoro, ambapo Bi. Matinde aliwaaelezea wanadiaspora wasisahu pia kuekeza nyumbani kwani nako kuna fursa nyingi hivyo ni muhimu kwa wanadiaspora kuangalia namna gani na wao wanaweza kunufaika na fursa hizo.

Wajumbe pia walipata fursa ya kuonyesha na kutangaza biashara zao kwa wafanyabiashara wa Comoro ambapo walionyeshwa kuvutiwa sana na bidhaa za kutoka Tanzania. Ikumbukwe kwamba Comoro ni nchi ambayo hutegemea kwa kiasi kikubwa bidhaa zake kutoka nje.

Biashara kati ya Tanzania na Comoro imekuwa ikikuwa siku hadi siku hata hivyo, bado kuna mahitaji makubwa ya bidhaa za chakula na imeonekana kuwa Tanzania ndio nchi iliyo katika nafasi nzuri kukidhi mahitaji hayo, kutokana na ukaribu wa nchi hizo kijiografia na kimila.

wajasiriamali wa Komoro wakiangalia bidhaa kutoka Tanzania

Wajasiriamali wa Comoro wakiangalia bidhaa kutoka Tanzania

Sambamba na hilo, kikundi cha wajasirimali wanawake kutoka Tanzania wanatarajia kutiliana saini mkataba wa ushirikiano (Memorandum of Understanding) baina yao na vikundi mbalimbali vya wajasiriamali wa Comoro.

Katika maelezo yake, Balozi wa Tanzania nchini Comoro, Mhe. Chabaka Kilumanga alieleza kuwa huu ndio wakati muafaka wa vikundi hivyo vikaanza kufanya kazi kwa pamoja na kujuana ili kuweza kuboresha na kukuza wigo wa biashara kati ya Tanzania na Comoro. Alieleza pia kuwa ubalozi utaaendelea kushirikiana na wanadiaspora iwapo watapendelea kufanya kazi kwa pamoja na wajasirimali hao.

Share:

Leave a reply