Wakuu wa nchi za Afrika Mashariki kukutana kesho Dar

631
0
Share:

Wakuu wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki wanatarajia kufanya mazungumzo ya pamoja baina yao katika Mkutano wa kawaida wa 18 utakaofanyika kesho Mei 20 Ikulu jijini Dar es salaam.

Mkutano huo unatarajiwa kupokea ripoti ya usuluhishi ya kamati inayoongozwa na Rais Mstaafu wa awamu ya tatu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Benjamin William Mkapa kuhusu mgogoro wa nchini Burundi.

Mambo mengine yatakayozungumzwa katika mkutano huo ni pamoja na taarifa na maelekezo mbalimbali yaliyotolewa katika mkutano wa 17 wa Wakuu wa nchi za Jumuiya hiyo.

Masuala hayo ni pamoja na namna ya kuwezesha uundaji wa magari katika Jumuiya ya Afrika Mashariki na kupunguza uagizaji wa magari yaliyotumika kutoka nje ya Jumuiya, mapitio kuhusu sekta ya nguo na ngozi.

Aidha masuala mengine ni pamoja na kuzuia ama kuondoa uagizaji wa nguo na viatu vilivyotumika kutoka nje.

Wakuu hao wa Nchi pia wanatarajia kujadili namna endelevu ya uchangiaji wa bajeti ya Jumuiya hiyo kwa nchi wananchama.

Aidha, katika Mkutano huo wa 18 Tanzania itakabidhi nafasi ya mwenyekiti wa Jumuiya hiyo iliyoishika kwa muda wa miaka miwili kwa nchi ya Jamhuri ya Uganda.

Na Immaculate Makilika- MAELEZO

Share:

Leave a reply