Walimu watakiwa kutenga muda wa ziada ili kuwafundisha wanafunzi elimu ya afya ya uzazi

349
0
Share:

SERIKALI  wilayani Sikonge mkoani Tabora,imewaagiza walimu shule za msingi na sekondari,kutenga muda kwa ajili ya kuwaelimisha (afya ya uzazi) wanafunzi wa kike juu ya vipindi vya ukuaji wa miili yao, ili kuwajengea mazingira mazuri ya kujilinda baada ya kufikia kipindi cha kubalehe.

Imedaiwa kwa njia hiyo,itasaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza maambukizo ya magonjwa ya zinaa, na mimba zisizotarajiwa kwa wanafunzi hao.

Agizo hilo limetolewa  na Mkuu wa wilaya ya Sikonge, Peres Boniphace Magiri,wakati akizungumza kwenye hafla ya makabidhiano ya msaada wa madawati 50 yenye thamani ya shilingi milioni tano, yaliyotolewa na NMB benki tawi la Sikonge kwa shule ya msingi Kiyombo.

Alisema miili ya binadamu na hususani ya watoto wa kike, inabadilika kadri ya miaka inavyozidi kusonga mbele, ambapo inafika wakati msichana ana balehe na kuanza kupenda vitendo vya ngono.

 “Ili kuepukana na vitendo hivyo, mwanafunzi wa kike anapaswa awe ameelimishwa mbinu bora za kukabiliana na mihemuko ya aina mbalimbali inayochochea kufanya ngono.Pia waelemishwe juu ya madhara yanayoweza kusababishwa na vitendo hivyo”, alisema na kuongeza kwa kusema;

“Mkoa wa Tabora ni wa kwanza kwa mambo ya ovyovyo yakiwemo ya mimba kwa wanafunzi na wasichana wenye umri chini ya miaka 18,kadhalika kwenye mitihani ya kitaifa ya darasa la saba,umekuwa wa mwisho kwa miaka mitatu mfululizo.Vile vile  ni wa mwisho kwa mambo ya msingi yakiwemo ya maendeleo ya wananchi wake”.

Peres Boniphace Magiri

Mkuu wa wilaya ya Sikonge mkoani Tabora, Peres Boniphace Magiri, akizungumza kwenye hafla ya makabidhiano ya msaada wa madawati 50 yenye thamani ya shilingi milioni tano yaliyotolewa msaada na NMB tawi la Sikonge.Kulia ni Meneja NMB tawi la Itigi,Victor Dilunga anayefuata ni Meneja NMB tawi la Sikonge, Stewart Singo. Wa tatu kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji halmashauri ya wilaya ya Sikonge,Simon Ngatunga akiteta na diwani wa kata ya Kiyombo.

Akiijengea nguvu hoja yake hiyo,Magiri alisema kuwa tatizo la mimba zisizotarajiwa kwa wanafunzi wa kike wilaya ya Sikonge na mkoa wa Tabora kwa ujumla,ni kubwa na linachangia kuharibu matarajio ya wanafunzi wa kike kufika mbali kielimu.

 Aidha,Magiri amewataka  walimu  wawe mfano kwa kuacha vitendo vya kujihusisha kimapenzi na wanafunzi wao wa kike.Wakati huo huo,wawachunge mienendo ya wanafunzi hao wa kike.

Katika hatua nyingine, Mkuu huyo wa wilaya, alisema mikutano ya hadhara katika wilaya hiyo ya kuhamasisha wananchi kujiletea maendeleo, itafanywa na viongozi waliochaguliwa katika maeneo yao tu, na si vingenevyo.

 Kwa upande wake Meneja wa NMB kanda ya magharibi, Leon Ngowi,,alisema NMB katika mipango yake,imekuwa ikishiriki shughuli mbalimbali za kijamii,husasani kwenye sekta ya elimu,afya na pia kufariji jamii pindi wanapopatwa na majanga kama mafuriko na ajali za barabarani.

Meneja NMB tawi la Sikonge mkoani Tabora, Stewart Singo

Meneja NMB tawi la Sikonge mkoani Tabora, Stewart Singo, akitoa taarifa ya msaada wa madawati 50 yenye thamani ya shilingi milioni tano yaliyotolewa na tawi hilo lwa shule ya msingi ya Kiyombo halmashauri ya wilaya ya Sikonge mkoani Tabora. Meneja Singo alitoa taarifa hiyo kwa niaba ya Meneja NMB kanda ya masgharibi,Leon Ngowi. Wa pili kulia aliyekaa ni Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Sikonge, Simon Ngatunga.

“Kwa mwaka huu, NMB imetenga zaidi ya shilingi bilioni moja kwa ajili ya kuchangia maendeleo ya wananchi kwenye sekta ya elimu na afya. Kiasi hiki kinatufanya kuwa benki  ya kwanza katika kuchangia maendeleo kuliko benki yoyote nchini.Kwa msaada huu wa madawati,ni sehemu ya benki yetu kumuunga mkono Rais Magufuli,kutimiza ahadi yake ya elimu bure”,alisema.

Aidha,Meneja Ngowi ambaye taarifa yake ilitolewa kwa niaba yake na Meneja NMB tawi la Sikonge,Stewart Singo,ametumia fursa hiyo, kuwahimiza walimu wakuu wa shule za msingi Bangayegya,  Lulanga na wenyeviti wa kamati za shule,kuhakikisha shule hizo zinapata mafanikio ya hali ya juu kielimu na hivyo, kuwa mfano bora hapa nchini.

Wakati huo huo, Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Sikonge,Simon Ngatunga,amewataka walimu kutekeleza majukumu yao kikamilifu,ili wawe na haki ya kudai stahiki zao.

Aidha,Ngatunga aliahidi kuanzisha utoaji wa tuzo kwa shule zitakazofanya vizuri kwenye mitihani ya kitaifa,lengo likiwa ni kuchochea maendeleo ya sekta ya elimu katika halmashauri hiyo.

Na Nathaniel Limu, Sikonge

Simon Ngatunga

Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Sikonge, Simon Ngatunga, akizungumza kwenye hafla ya makabidhiano ya msaada wa madawati 50 yenye thamani ya shilingi milioni tano yaliyotolewa na NMB tawi la Sikonge kwa shule ya msingi Kiyombo. Pamoja na mambo mengine, Ngatunga amewahimiza walimu kufanya kazi kwa moyo na kujituma, ili waweze kujijengea mazingira mazuri ya kuendelea kulipwa stahili zao.Wa kwanza kulia ni Mkuu wa wilaya ya Sikonge, Peres Boniphace Magiri.Kushoto ni wajumbe wa kamati ya shule pamoja na mjumbe wa kamati ya ulinzi.

Mkuu wa wilaya ya Sikonge mkoani Tabora, Peres Boniphace Magiri

Mkuu wa wilaya ya Sikonge mkoani Tabora, Peres Boniphace Magiri, akikata utepe kuathiria makabidhiano ya msaada wa madawati 50 yenye thamani ya shilingi milioni tano yaliyotolewa msaada na NMB tawi la Sikonge kwa shule ya msingi ya Kiyombo.

Stewart Singo

Meneja NMB tawi la Sikonge mkoani Tabora, Stewart Singo (kulia) akimkabidhi mkuu wa wilaya ya Sikonge,Peres Boniphace Magiri, madawati 50 yenye thamani ya shilingi milioni tano yaliyotolewa msaada na benki hiyo kwa shule ya msingi Kiyombo.

wanafunzi wa shule ya msingi Kiyombo

Baadhi ya wanafunzi wa shule ya msingi Kiyombo wilaya ya Sikonge mkoani Tabora,wakifurahia msaada wa madawati 50 yenye thamani ya shilingi milioni tano yaliyotolewa msaada na NMB tawi la Sikonge.(Picha zote na Nathaniel Limu).

Share:

Leave a reply