Wanafunzi wa kike washauriwa kusoma masomo ya sayansi kutokana na uwepo wa fursa za ajira

275
0
Share:

Imeelezwa kuwa watoto wa kike wana nafasi kubwa ya kutimiza ndoto zao endapo wataamua kutoyakimbia masomo ya sayansi kutokana na sekta ya sayansi kuwa na wigo mpana wa fursa za kuajiriwa na kujiajiri ukilinganisha na sekta nyingine.

Hayo yameelezwa na wahitimu wa kidato cha nne 2016 katika Shule ya Mwilamvya Sekondari iliyopo wilayani Kasulu, wakati wa mahafali ya tisa ya kidato cha nne shuleni hapo.

Mmoja wa wahitimu hao Tausi Athumani, amewashauri vijana wenzake hususani wa kike wapende sana masomo ya Sayansi kwani upo ushahidi kwamba wasichana waliothubutu kusoma masomo ya sayansi wamepata mafanikio na pia wamekuwa msaada mkubwa katika jamii.

Aidha wahitimu hao wa kidato cha nne pia wamesema kuwa ili mtoto aweze kutimiza ndoto zake yampasa alelewe katika maadili tangu akiwa mdogo na kwamba kama wazazi nyumbani hawatawalea watoto katika maadili hawawezi kufanya miujiza wakiwa na walimu shuleni.

Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Kasulu, Scarion Ruhula, ambaye alikuwa mgeni rasmi akimwakilisha Mkuu wa Wilaya kwenye mahafali hayo amewasihi wazazi na walimu wote kuwa wana jukumu la malezi ya watoto ili wakaishi vizuri katika jamii hata baada ya kumaliza masomo yao.

Awali Mkuu wa Shule ya Sekondari Mwilamvya, Mwalimu Emmanuel Saguda, ameeleza kuwa walimu wakati mwingine hulazimika kuwarudisha nyumbani watoto kutokana na mienendo isiyofaa ambayo husababisha walimu kuegemea malezi zaidi kuliko taaluma.

Amesema matumizi ya simu, uvaaji wa milegezo kwa wanafunzi shuleni huchangia kwa kiasi kikubwa kutofanya vizuri katika masomo yao.

Katika hatua nyingine, mkuu huyo wa shule ameiomba serikali iziunguzie kodi shule binafsi kwani zina mchango mkubwa kwa taifa lakini zinalipa kodi nyingi huku serikali ikiwa haizipi ruzuku kama ilivyokuwa katika miaka ya 80 na 90.

Jumla ya wanafunzi 119 wanategemea kuhitimu kidato cha nne mwaka huu katika shule ya Mwilamvya Sekondari iliyoko wilayani Kasulu mkoani Kigoma.

Share:

Leave a reply