Wanahabari watakiwa kufanya utafiti wa mafuta na gesi asilia

632
0
Share:

Mkuu wa Wilaya ya Iringa (DC), Richard Kasesela avitaka vyombo vya habari nchini kutenga mafungu kwa ajili ya utafiti  ukiwemo wa mafuta na gesi asilia.

Alisema kuwa masuala ya mafuta na gesi asilia yamepotoshwa kwa muda mrefu kutokana na wanahabari na vyombo vya habari kutowekeza katika utafiti, jambo ambalo linafanya wanahabri wengi kukwepa kuandika habari za utafiti au kupotosha jamii kwa lengo ya kuuza habari.

DC Kasesela alitoa rai hiyo wakati wa mafunzo kwa waandishi wa habari ya namna ya kuandika masuala ya mafuta na gesi asilia yaliofanyika hivi karibuni mkoani Iringa.

Mafunzo hayo yalianaliwa na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) kwa kushirikisha mikoa ya Njombe, Ruvuma na Iringa.

Alisema kuwa changamoto kubwa ya baadhi ya wanahabari huwa hawataki kujishughulisha na utafiti, kwani utafiti una gharama zake, jambo ambalo linafanya wanahabari wengi kukwepa kuandika habari za utafiti au kupotosha jamii ili mradi kuuza habari.

“Vyombo vyetu vya habari havitoi fungu la utafiti jambo ambalo linafanya vyombo vingi vya habari aidha kukwepa kuandika habari hizi au kuandika kwa kupotosha jamii ili mradi auze habari,” alisema Kasesela.

Alisema kuwa ili kuhakikisha na kuimarisha ushiriki wa wananchi katika shughuli za sekta ndogo ya mafuta na gesi asilia katika mkondo wa juu, kati na wa chini, vyombo vya habari havinabudi kutenga mafungu kwa ajili ya utafiti.

Alisema kuwa wanahabari nchini hawanabudi kuhabarisha jamii ili iweze kujua manufaa ya uwepo wa mafuta na gesi asilia ili wachangamkie fursa.

Mwaka 2015 Bunge la awamu ya nne ilipitisha sheria mpya kwa ajili ya kusimamia sekta ndogo ya mafuta nchini kwenye masuala ya utafitaji, uendelezaji, uzalishaji, usafirishaji, uingizaji, uchakaji, uhifadhi na biashara ya mafuta na gesi asilia nchini.

DC huyo alisema kuwa sheria hiyo ya mwaka 2015 imekuja kwa wakati muafaka ikiwa na nia njema ya kuhakikisha rasilimali hiyo inanufaisha taifa kwa ujumla.

Lengo likiwa ni kuhakikisha sekta ya mafuta nchini inakuwa endelevu na kulinda maslahi ya wadau wote kwa ustawi wa taifa na watanzania kwa ujumla.

Na Friday Simbaya, Iringa

Share:

Leave a reply