Wanahabari watakiwa kutumia taaluma yao kuelimisha jamii kuhusu ukeketaji

265
0
Share:
Waandishi wa habari mkoani Singida, wamehimizwa kutumia taaluma yao kuielimisha jamii juu ya madhara yanayosababishwa na vitendo vya ukeketaji, ili pamoja na mambo mengine, mkoa uweze kuondoka kwenye kundi la mikoa mitano nchini inayoongoza kwa ukeketaji.

Hayo yamesemekana juzi na Kaimu mtendaji shirika lisilo la kiserikali la Empower Society, Transform lives (ESTL) Rose Mjema, wakati akitoa mada yake kwenye semina kwa waandishi wa habari, iliyohusu vita vya mapambano dhidi ya ukeketaji.

Alisema ukeketaji wenye madhara mengi ikiwemo vifo, unachangiwa kwa kiasi kikubwa na mila na desturi ambazo zimepitwa na wakati.

“Mkoa wa Singida ambao upo kwenye kasi nzuri katika kusukuma gurudumu la maendeleo, haupaswi kuendekeza mambo ambayo yamepitwa na wakati. Pia yenye madhara mengi. Vita ya kutokomeza mila na desturi inayoendelezwa hadi ukeketaji hadi kwa watoto wachanga wa kike, itakuwa nyepesi endapo vyombo vya habari vitashiriki kikamilifu vita hivyo kupitia taaluma yao,” alifafanua Rose.

Akisisitiza, alisema juhudi za waandishi wa habari zitakuwa na tija zaidi kwenye vita hii, iwapo kupitia taaluma yao wataandika kwa jicho la kijinsia, na ushawishi utakaosaidia wananchi kuchukia ukeketaji.

Akisisitiza zaidi, kaimu mtendaji huyo,amewataka wahakikishe wanakuwa na uelewa wa kina na mpana, juu ya madhara ya ukeketaji ya muda mfupi na muda mrefu.

Rose  ametaja baadhi ya madhara ya papo kwa papo/muda mfupi, kuwa ni maumivu makali, kupoteza damu nyingi, pepopunda na maambukizi ya vijidudu ambavyo huweza kuasbabisha kifo.

Aidha,ametaja, baadhi ya madhara ya muda mrefu kuwa ni pamoja na UTI za mara kwa mara, makovu sugu, uvimbe, utasa, matatizo wakati wa kujifungua na kushidwa kufurahia tendo la ndoa (maumivu makali wakati wa kujamiiana)

Kwa mujibu wa kaimu mtendaji huyo, zaidi ya watoto wa kike na wanawake milioni 125 duniani kote wamefanyiwa ukeketaji.

Kwa upande wa Tanzania, katika kila wanawake 100, wanawake 15 wamekeketwa (inakadiriwa wanakaribia million 8).

Kitaifa ukeketaji unapungua lakini kwa mkoa wa Singida, tatizo linaongezeka. Mikoa inayoongoza kwa ukeketaji ni Manyara, Dodoma, Arusha, Singida, Mara na Shinyanga.

Makabila yanayoongoza ni Wanyaturu,Wagogo,Wamasai,Wapare, Wakuria ,Wahadzabe, Wabarbaig na Wambulu.
Na Nathaniel Limu, Singida
Share:

Leave a reply