Wanahabari watakiwa kuunganisha nguvu zao katika mapambano dhidi ya majangili nchini

251
0
Share:
Clement Matwinga

MKURUNGENZI  wa Shirika lisilo la Kiserikali la Rafiki Wildlife Foundation, Mchungaji Clement Matwinga, amewahimiza waandishi wa habari nchini kuunganisha nguvu zao na wadau wengine, ili kuharakisha kutokomeza matukio ya ujangili yanayotishia kutoweka kwa wanyamapori.

Mchungaji Matwinga ametoa wito huo wakati akizungumza kwenye kilele cha maadhimisho ya siku ya wanyamapori duniani, iliyofanyika kwenye uwanja wa Namfua mjini hapa.

Alisema rasilimali ya wanyamapori ni mali ya Watanzania wote na siyo ya majangili, hivyo kila Mtanzania wakiwepo na waandishi wa habari, wanalo jukumu la kulinda wanyamapori wasivunwe ovyo.

“Kama tunavyofahamu kwamba Wanyamapori hawawezi kujilinda, jukumu la kuwalinda ni la kila Mtanzania kwa nafasi yake. Tuhakikishe tunawalinda kama tunavyolinda mifugo yetu,tufanye hivyo kwa faida ya kizazi chetu kile kijacho” alisema Mchungaji Matwinga.

Parseko Kone

Mkuu wa mkoa wa Singida, Dk.Parseko Vicent Kone, akizungumza kwenye hafla ya kilele cha maadhimisho ya siku ya wanyamapori duniani yaliyofanyika kwenye uwanja wa Namfua mjini hapa.

Alifafanua kwa kusema kuwa “waandishi wa habari wanayo nafasi nzuri ya kuelimisha jamii kupitia makala na habari mbalimbali juu ya madhara yatokanayo na uwindaji haramu. Kwa njia hiyo, watakuwa wanaitikia vema kauli mbiu ya mwaka huu ya “Hatima ya wanyamapori ipo mikononi mwetu”.

Hata hivyo, Mchungaji huyo, alitumia fursa hiyo kupongeza vyombo vya habari kwa kazi nzuri ya kupiga vita dhidi ya ujangili na amevitaka  visichoke mbali viongeze juhudi zaidi, kwa lengo la kukomesha uwindaji haramu.

Kwa upande wa Waziri Wizara ya Maliasili na Utalii katika hotuba yake iliyosomwa kwa niaba yake  na Afisa wanyamapori mkuu kitengo cha uenezi idara ya wanyamapori, Twaha Twaibu, alisema Wizara ikishirikiana na wadau mbalimbali wa uhifadhi, inafanya juhudi za makusudi, kuhakikisha ujangili unakoma.

Twaha Twalibu

Afisa wanyamapori Mkuu kitendo cha uenezi idara ya wanyamapori makao makuu, Twaha Twalibu, akitoa taarifa ya utekelezaji ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwenye kilele cha maadhimisho ya siku ya wanyamapori duniani yaliyofanyika mkoani Singida.

Aidha, alisema Wizara imejiwekea mikakati ya kupambana na ujangili ambayo ni pamoja na kuendelea kutoa elimu ya uhifadhi wa wanyamapori na mafunzo ya intelejensia.

Mgeni rasmi katika maadhimisho hayo Mkuu wa mkoa wa Singida, Dk. Parseko Kone, amewataka wananchi wa mkoa wa Singida, kuheshimu sheria za uhifadhi na pia wasijaribu kabisa kuingiza  mifugo yao  kwenye maeneo yaliyohifadhiwa.

“Natoa wito wananchi wote kuunga mkono juhudi zinazofanywa na serikali hii ya awamu ya tano kwa kauli yake ya mbiu yake ya “Hapa kazi tu”, kupitia hatma ya wanyamapori ipo mikononi mwetu, hivyo ni jukumu la kila Mtanzania kulinda na kuhifadhi Wanyamapori wetu”, alisema.

siku ya wanyamapori duniani

Baadhi ya viongozi wa madhehebu ya dini mkoani Singida wakimsikiliza Mkuu wa mkoa wa Singida, Dk.Parseko Kone,waliohudhuria kilele cha maadhimisho ya siku ya wanayapori dunaini yaliyofanyika mkoani Singida.

Rafiki Wildlife Foundation

Bango la Rafiki Wildlife Foundation.(Picha na Nathaniel Limu).

Share:

Leave a reply