Wasaidizi wa Lazaro Nyalandu wagoma kuhama CCM

364
0
Share:

Wasaidizi watatu wa karibu na aliyekuwa mbunge wa jimbo la Singida Kaskazini, Lazaro Nyalandu, wameahidi wataendelea kuwa watiifu na waaminifu kwa CCM na kwamba kuanzia sasa, hawana urafiki tena na Nyalandu.

Wasaidizi hao wameyasema hayo juzi kwa nyakati tofauti mbele ya kamati ya siasa mkoa,wajumbe wa halmashauri CCM wilaya ya Singida na baadhi ya wana CCM wilaya ya Singida.Kikao hicho maalum kimefanyika katika kijiji cha Ilongero.

 Diwani wa viti maalum tarafa ya Mtinko,Hadiha Kisuda,amesema kuwa amesikitishwa na maamuzi ya Nyalandu kwa kitendo chake cha kushindwa kuwashirikisha wazaidizi wake, au watu wa karibu naye.

Akisisitiza, Hadija alisema mtu yeyote mwenye hekima na busara, katika maamuzi ya aina ya Nyalandu, ni lazima ashirikishe watu wa karibu naye.Ili waweze kumshauri kama yanafaa au laa.

Alisema siku mbili kabla ya Nyalandu kutoa maamuzi yake, walifanya ziara naye katika sekondari ya Mtinko na aliahidi kuzifanyia kazi changamoto zinazoikabili shule hiyo.

Diwani huyo alisema matendo na maneneo aliyokuwa akiyatenda na kusema wakiwa kwenye shule hiyo,yalikuwa sio ya kawaida. Kitendo hicho kilisababisha  hofu ya aina yake kwa watu wanao mfahamu kwa muda mrefu.

“Alipoondoka Mtinko,tuliobaki tukaanza kujiuliza mbunge wetu kapatwa na nini mbona hayupo kwenye hali yake tuliyoizoea?, Baada ya siku mbili kupita, Nyalandu alitoa maamuzi hayo magumu.Nilipigiwa simu nyingi mno, naulizwa mtu wako kapatwa na nini,” alisema kwa masikitiko makubwa na kuongeza.

“Baada ya kujiridhisha juu ya Nyalandu kujivua ubunge na uana CCM,mwili wote ulitoka jasho na nilikunywa zaidi ya lita sita za maji”.

Naye msaidizi mwingine ambaye pia ni mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Singida, Elia Digha, alisema alifahamiana na Nyalandu mwaka 2000 akiwa amevaa kaptula. 

“Toka wakati huo hadi juzi kabla hajatoa maamuzi yake,nilikuwa mtu wa karibu naye kuliko mtu ye yote wa jimbo la Singida kaskazini. Nyalandu hakuwa na mbinu kabisa zinazohusu uchaguzi. Kila kitu kuhusu uchaguzi wa wabunge, nilikuuwa nazifanya mimi, yeye anakuja siku saba kabla ya uchaguzi. Na alikuwa akizoa kura za kutosha,” alisema Digha.

Alisema Nyalandu ameondoka CCM ameiacha imara, na itaendelea kuwa imara bila yeye kuwepo.

Aliyekuwa Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Singida, Narumba Hanje, alisema juzi juzi Nyalandu alimwahidi kuwa wakati wo wote atafanya mkutano mkubwa wa jimbo ili pamoja na mambo mengine, watafanya tathimini ya maendeleo ya jimbo hilo.

“Wakati anatoa ahadi hiyo, kumbe Nyalandu alikuwa na yake moyoni, ghafla tukasikia amejivua uanachama wa CCM na ubunge. Tusihangaike na Nyalandu, sisi tutaendelea kubaki CCM na jimbo la Singida Kaskazini litaendelea kuwa chini ya CCM daima,” alisema Hanje.

Katika hatua nyingine, Mwenyekiti wa UWT mkoa wa Singida, Diana Chilolo, alisema katika kipindi chake cha ubunge, hajawahi kumsikia Nyalandu akiwasilisha bungeni kero za wapiga kuwa wake kwa muda wote alikuwa bubu.

“Nyalandu hakuwa mwakilishi mzuri wa wapiga kura wake bungeni. Pia hata nje ya bunge nako hajawatumikia ipasavyo. Akipanda jukwaani kwenye jimbo lake ataongea chini ya dakika tano anashuka. Alikuwa anawaacha midomo wazi wapiga kura wake na wananchi wengine kwa ujumla, kwa vile anakuwa hana la maana alilowaambia wananchi,” alifafanua.

Chilolo alisema kuwa kama ni fundisho,Nyalandu ameisha toa fundisho tena sio kwa jimbo la Singida kaskazini tu ni kwa majimbo yote nchini.

“Ni lazima sasa CCM kwenye jimbo hili ijipange vizuri kwa kumchangua mbunge ambaye atakwenda na kasi ya utendaji ya rais Magufuli,” alisema Chilolo na kushangiliwa kwa nguvu.

Na Nathaniel Limu, Singida

Share:

Leave a reply