Watano wapoteza maisha katika ajali ya basi la Lupondije Express, Iringa

242
0
Share:

Usiku wa siku ya Pasaka umekuwa mbaya kwa baadhi ya familia nchini kufuatia kutokea kwa ajali ya basi la Lupondije Express lililokuwa likitokea Mwanza kuelekea Iringa na kusababisha vifo vya watu watano.

Akizungumza na Mo Blog, Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Iringa, Peter Kakamba  (pichani) amesema ajali hiyo imetokea katika eneo la Ipogolo majira ya saa 3:30 usiku wakati basi la Lupondije Express lenye namba T798 AKV likielekea Iringa kwa ajili ya kuwabadilishia abiria basi waliokuwa wanaelekea Mbeya.

Kamanda Kakamba amesema katika ajali hiyo watu watano wamepoteza maisha, wanawake wakiwa watatu na wanaume wawili pia abiria 38 kupata majeruhi ambapo baada ya kupatiwa matibabu abiria 11 waliruhusiwa kutoka hospitali na wengine 27 kubaki hospitali kwa matibabu zaidi.

“Kuna ajli ndiyo ilitokea jana usiku katika eneo la Ipogolo eneo lile lina kona nyingi kwahiyo wakati wakiwa wanapita eneo hilo wakawa wamepata ajali na abiria watu watano wamepoteza maisha palepale,” amesema Kamanda Kakamba.

Aidha Kamanda ametaja chanzo cha ajali hiyo kuwa ni uzembe wa dereva wa basi hilo kukosa umakini na kusababisha ajali ambayo imegharimu maisha ya watanzania na baada ya kutokea ajali dereva alitimkia kusipojulikana, hivyo Polisi wanaendelea kumtafuta.

Share:

Leave a reply