Watanzania watakiwa kuwa na utaratibu wa kukagua miradi ya maendeleo katika maeneo yao

307
0
Share:

Mkurugenzi wa mipango wa shirika lisilo la kiserikali la WaterAid Tanzania, Abel Dugange, ametoa rai kwa serikali ya mkoa wa Singida kujenga utamaduni wa kukagua shughuli za miradi na huduma zinazotolewa na mashirika yasiyo ya kiserikali (NGos) na wadau wengine ili kubaini kama zinawiana na mikakati ya mkoa.

Akisisitiza, amesema kwa njia hiyo,kutaondoa uwezekano wa miradi ya maendeleo au huduma za aina moja kutekelezwa katika eneo moja na NGos au wadau zaidi ya moja. Huku maeneo mengine mengi, yakiwa hayana NGos wala mdau wa kuwasaidia kuwaletea miradi ya maendeleo.

Aidha, alisema upo umuhimu mkubwa kwa serikali ya mkoa, halmashauri za wilaya na manispaa kuwa na ratiba ya kukutana mara kwa mara na NGos na wadau wa maendeleo mkoani hapa ,ili kubadilishana uzoefu na kuweka mikakati ya kusogeza mbele maendeleo ya wananchi.

Mkurugenzi Dugange ametoa rai hiyo juzi wakati nasaha zake kwenye hafla ya makabidhiano ya miradi mbalimbali iliyotekelezwa na shirika lisilo la kiserikali la SEMA katika halmashauri ya wilaya ya Iramba na manispaa ya Singida.

“Kama sote tutafanya kazi kwa mfumo wa mnyororo mmoja na kuwa wabunifu wazuri katika majukumu yetu,mkoa wa Singida,utakuwa mfano wa kuigwa na mikoa mingnine kwa maendeleo yake.Itafika wakati NGOs zitafunguka na kuwa na ushirikiano wa dhati katika kuwatumikia wananchi wa mkoa huu,” alisema.

Aidha, Dugange alisema umefika wakati sasa kuwajibisha baadhi ya watendaji wa umma ambao wamekuwa kikwazo kwa wafadhili na wadau ambao wamekuwa wakijitolea kuondoa kero zinazowakabili wananchi.

Katika hatua nyingine, alisema kwa muungano huo,pamoja na faida zake nyingi,pia itasaidia kuwawezesha wananchi kumiliki miradi yao inayotekelezwa na wafadhili na wadau wengine wa maendeleo.

Mkurugenzi huyo alisema miradi mingi inayotekelezwa na mashirika yasiyo ya kiserikali na wadau wengine imekuwa ikigharimu fedha nyingi na wafadhili wamekuwa wakilenga miradi hiyo inufaishe wananchi kwa kipindi kirefu.

“Lengo hilo la miradi kunufaisha wananchi kwa muda mrefu, limekuwa halifikiwi kutokana na wananchi kutokutambua kuwa miradi hiyo ni mali yao na wanapashwa kuilinda na kuitunza,” alisema na kuongeza;

“Ili wananchi waweze kutambua kuwa miradi hiyo ni mali yao,kwanza waelimishwe na washirikishwe kuanzia maadalizi ya miradi au huduma,waweze kushiriki kikamilifu katika utekelezaji wake.Kwa njia hiyo, miradi itadumu kwa muda mrefu”.

Kwa upande wake kaimu mkuu wa mkoa wa Singida, Elias Tarimo,alisema wazo la kuratibu shughuli za NGOs,wamelipokea na watalifanyia kazi.

Share:

Leave a reply