Wateja wa NMB sasa kutuma pesa benki nyingine kwa kutumia NMB Mobile

743
0
Share:

NMB imezindua rasmi huduma ya kuhamisha ama kutuma fedha (NMB Mobile T.I.S.S), kutoka katika akaunti za benki hiyo, kwenda kwenye akaunti za benki nyingine, sambamba na kufanya manunuzi na malipo.

NMB Mobile T.I.S.S, ni huduma ya kwanza kutolewa na benki nchini Tanzania, ambayo imetajwa kuwa ni njia rahisi, salama na ya haraka katika mchakato wa kutuma ama kuhamisha fedha kutoka NMB kwenda benki nyingine.

Akizungumza katika hafla ya kuitambulisha huduma hiyo kwa wanahabari, Kaimu Meneja Mwandamizi wa Amana, Huduma za Bima na Huduma za Ziada, Stephen Adili Adili alisema NMB Mobile T.I.S.S ni mwarobaini wa wateja wao kutumia muda mrefu kwenye foleni za kuhamisha ama kutembea na fedha mkononi.

“Huduma hii inakuja kumaliza tatizo la wateja kutumia muda mwingi kwenye mchakato wa kuhamisha fedha. Muda ni mali na kwa kulitambua hilo, tumekuja na huduma hii ambayo inafanyika popote, hata ukiwa ufukweni unapunga upepo,” alisema Adili.

Aliongeza ya kwamba, NMB Mobile T.I.S.S haiishii tu katika kuhamisha fedha kutoka akaunti ya NMB kwenda benki nyingine, bali inaenda mbali na kupokea ama kutuma miamala ya mitandao ya simu za mkononi.

Huduma hiyo inayoweza kutumiwa na wateja wa NMB Mobile, inapatikana kwa mteja kubonyeza alama nyota, kisha namba 150, alama ya nyota, kisha namba 66 na mwisho alama ya reli na kufuata maelekezo (*150*66#)

Naye Geofrey Mwijage, ambaye ni Mkuu wa Uendeshaji wa Shughuli za Kibenki wa NMB, alisema benki yake imejidhatiti vya kutosha katika kutanua huduma mongoni mwa wateja wao na Watanzania kwa ujumla.

Alisema NMB Mobile T.I.S.S ni inaenda kuwa mshirika sahihi wa Watanzania, katika kuharakisha maendeleo yao na kukuza pato la mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla kuelekea Tanzania ya Viwanda.

Share:

Leave a reply