Watu wavivu hatarini kupata yasiyo ya kuambukiza

359
0
Share:

Kufuatia ongezeko la idadi ya wagonjwa wa magonjwa yasiyo ya kuambukiza ikiwemo kansa, shinikizo la damu na hata tatizo la ukosefu wa nguvu za kiume na wanawake kuzaa watoto wenye migongo wazi na vichwa vikubwa.

Daktari wa Afya ya Jamii na Familia, Dkt. Ally Mzige ametaja viashiria hatarishi vipya ambavyo ni vigeni katika masikio ya watu, vinavyosababisha magonjwa na matatizo hayo. Mzige ametaja vihatarishi hivyo leo Mei 19, 2017 jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari.   

Vihatarishi alivyotaja ni pamoja na, kitendo cha mtu kukaa muda mrefu bila kufanya kazi. Anaeleza kuwa, mtu kukaa kwa zaidi ya saa nne bila kufanya kazi athari yake ni sawa na mtu aliyevuta sigara 14 kwa siku, na hivyo ana uwezekano mkubwa wa kupata athari anayoipata mvutaji sigara ikiwemo magonjwa ya saratani na mapafu.

Kihatarishi kingine ambacho watu wengi hawakijui ni kutokula mboga za majani, ambapo kwa mujibu wa ripoti ya Shirika la Afya Duniani (WHO) watu takribani milioni 2.7 hufariki kila mwaka kwa sababu ya kutokula mboga za majani.Dkt. Mzige anaeleza kuwa, mwanamke kutokula mboga za majani kunapelekea kujifungua mtoto mwenye mgongo wazi na au kichwa kikubwa.   

Unene kupita kiasi, sambamba na uzito uliokithiri, ni miongoni mwa vihatarishi vilivyotajwa na Dkt. Mzige, ambavyo huathiri mifumo 13 ya mwanadamu na hupoteza uwezo wa mtu kutembea, na kusababisha maaumivu ya mgongo na viungo ya mara kwa mara.

“Mtu anapotembea kuna faida, mfano ukipiga hatua moja, ni sawa na kuishughulisha misuli 200. Lakini mtu mnene na mwenye uzito kupita kiasi hupoteza uwezo wa kutembea, huumia mgongo na viungo na kupata mshituko wa moyo. Ili kuepukana na tatizo hilo, ni vema kuwa na desturi ya kufanya mazoezi mara kwa mara na kula mlo uliokamilika wenye virutubishi na madini ya kutosha,” anasema.

Kwa upande wa tatizo la ukosefu wa nguvu za kiume linalokumba wanaume wengi, anasema kwamba sukari ambayo ina athari zaidi ya 146, ndio mzizi wa tatizo hilo ambayo hupunguza kwa kasi nguvu za kiume, bila kusahahu ulaji wa vyakula vya mafuta, ambapo amesema kwa kawaida mtu anatakiwa kula mayai 3 na nyama nusu kilo kwa wiki.

Na kwamba, hali hiyo ni tofauti na maisha ya sasa, kwani wengi wao hula vyakula vya mafuta kama chipsi, mayai, soseji, kuku na kadhalika. Hata hivyo, Mzige anasema, ulaji huo hauathiri nguvu za kiume pekee, bali husababisha kisukari cha mimba kwa wanawake.

Licha ya Dkt. Mzige kutaja vihatarishi hivyo, ameikumbusha jamii athari za unywaji  pombe kupita kiasi, inayosababisha magonjwa zaidi ya 60 na matatizo ya kisaikolojia 200. Na kwamba husababisha magonjwa ya kisukari, saratani ikiwemo ya ini, utumbo mpana na mifupa. 

Dkt. Mzige ameishauri jamii kupunguza nishati lishe ya ziada ikiwemo sukari, mafuta yenye lehemu na chumvi, pia kufanya mazoezi ya kimwili na akili mara kwa mara, pamoja na kupiga mswaki kwa kusafisha meno na ulimi,  kwa kuwa asilimia 60 ya watanzania wana afya duni katika mfumo wa afya ya kinywa kwa kutopiga mswaki.

 Na Regina Mkonde.  

Share:

Leave a reply