Wazanzibar waandamana nchini Canada kupinga kurudiwa kwa uchaguzi Visiwani Zanzibar

205
0
Share:
Na Mwaandishi wetu Washington 
 Wakati hali ya kisiasa Visiwani Zanzibar ikiwa inazidi kutokota, bila kujali theluji na baridi kali, Wazanzibari waishio nchini Canada mnamo tarehe 27 mwezi huu walifanya maandamano katika Mji Mkuu wa nchi hiyo, Ottawa katika juhudi za kutafuta uingiliaji kati wa kimataifa katika kusaka suluhisho la amani kwa mgogoro wa kisiasa Visiwani humo.
Mandamano ya Wazanzibari waishio nchini Canada wakiwa mwenye ofisi ya European Union  Mjini Ottawa
Wazanzibari hao waliandamana hadi kwenye Ofisi ya Waziri Mkuu wa Canada kwa lengo la kufikisha ujumbe wao kukhusiana na hali mbaya ya kisiasa huko Zanzibar.
Akizungumza na Swahilivilla, mmoja wa waandaaji wa maandamano hayo Bwana Zamil Rashid alisema kuwa lengo la maandamano hayo ni kuwaunga mkono ndugu zao Wazanzibari katika harakati za kudai demokrasia ya kweli na kupinga hatua za kufutwa kwa uchaguzi Mkuu Zanzibar.
“Madhumuni ya maandamano yetu yalikuwa ni kuwaunga mkono ndugu zetu wa Zanzibar kwa mambo yaliyofanyika, na kwamba hatukubaliani nayo” alisema Bwana Zamil na kuendelea “Wazanzibari walioko nchini Canada wanapinga jambo hilo lilofanywa na Serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na matamshi aliyoyatoa Bwana Jecha Salim Jecha ya kufuta uchaguzi”
Aidha maandamano hayo yalikuwa na lengo la kuiomba Serikali ya Canada kuingilia kati katika kuupatia ufumbuzi mgogoro wa kisiasa Visiwani Zanzibar kabla hali haijawa mbaya zaidi.
Mbali na Ofisi ya Waziri Mkuu wa Canada, Wazanzibari hao pia waliandamana hadi kwenye Ofisi za Umoja wa Ulaya nchini humo kwa dhumuni hilo hilo.
“Vilevile tumefikisha ujumbe wetu kwa Umoja wa Ulaya (EU) ili walishighulikie swala hili haraka iwezekanavyo kabla hayajatokea maafa kwa Wazanzibari”, alisema Bwana Zamil.
Katika Risala yao kwa pande zote mbili, waandamanaji hao wametoa wito wa kutangazwa mshindi badala ya kurejewa kwa uchaguzi kama ilivyotangazwa na Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) Bwana Jecha Salim Jecha. “Tumetoa wito wa yule aliyeshinda uchaguzi atangazwe, na siyo kurejea uchaguzi” alisisitiza Bwana Zamil. 
Kwa kufikisha ujumbe wao kwa Umoja wa Ulaya, wazanzibari hao pia walikuwa na lengo la kutoa wito kwa nchi nyengine duniani kusaidia katika kuupatia suluhu mzozo wa kisiaza Zanzibar, ikiwemo pia kusitisha missada ya kiuchumi kwa Tanzania.
Share:

Leave a reply