Waziri Lukuvi awatangazia kiama matapeli na viongozi serikali za mitaa

471
0
Share:

Waziri wa Ardhi Nyumba na Makazi, William Lukuvi amesema wanatarajia kupeleka mswada Bungeni mwezi Septemba, kwa ajili ya kufanya Marekebisho ya sheria ya ardhi, ili kudhibiti matapeli pamoja na kuondoa migogoro ya ardhi.

Vilevile amesema mabadiliko hayo yataruhusu uwepo wa Wakurugenzi Wasaidizi Mipango Miji kwenye kanda zote nchini, ili wananchi wapate huduma ya ardhi kwa haraka.

Lukuvi ameyasema hayo leo jijini Dar es Salaam wakati akitoa hati 4333 za wakazi wa Kata ya Kimara, ambapo amesema serikali itaendelea kuboresha huduma za usimamizi wa ardhi ili kuondoa migogoro.

“Mwezi huu kanda zote kutakuwa na mtu anaidhinisha michoro ya upangaji yote, tulikuwa tunayemthamini mmoja, lakini tumeteua wengine wanane, tutakuwa na wathamini katika kila kanda ili kuondoa migogoro na wananchi kupata huduma ya ardhi kwa haraka. Halmashauri msiruhusu watu kujenga kwenye maeneo yasitopimwa au kupangwa,” amesema.

Amesema Serikali itahakikisha inaondoa vikwazo vinavyochelewesha wananchi kujenga ikiwemo kuzuia ucheleweshaji wa vibali vya ujenzi na upimwaji wa ardhi.

“Tunataka kuondoa makazi holela kwa kufanya zoezi la urasimishaji makazi, watu wapewe fursa ya kujenga haraka,” amesema.

Katika hatua nyingine, amewaonya matapeli kwa kusema kuwa kiama chao kimewadia, na kuwataka viongozi wa serikali za mitaa kutoshirikiana na matapeli hao kudhurumu ardhi za wananchi.

“Baadhi ya wenyeviti ni matapeli hiyo tabia lazima ikome. Mnatumia mihuri yenu vibaya mnatoa taarifa kwa matapeli. Matapeli siku zao zimewadia, viongozi wa serikali za mtaa na watendaji wa ardhi mna ndoa na matapeli, tabia hiyo acheni. Na vyama vote mchinje matapeli sababu hatuwataki tunataka viongoz wenye kazi zao,” amesema.

Pia, Lukuvi amesema kuanzia sasa wenye maeneo makubwa yasiyoendelezwa pamoja na waliojenga katika viwanja visivyopimwa au katika makazi holela watapewa leseni za makazi za muda ili walipe kodi, wakati wakifuata taratibu za kupimiwa maeneo yao.

“Tunatoa ukomo wa muda kwa watakaopewa leseni za makazi kupima maeneo yao ili kupata hati, muda ukifika tutaagiza halmashauri kubomoa nyumba,” amesema.

Licha ya hayo, Lukuvi ameagiza mazoezi ya urasimishaji makazi kusimamiwa na wananchi kwa kushirikiana na halmashauri, badala ya Kamati za MipangoMiji za Manispaa ili kuondoa urasimu na mianya ya rushwa inayopelekea ucheleweshaji.

“Kamati za urasimishaji makazi za mitaa zisimamiwe na wananchi wenyewe, wapange miji kwa kushirikiana na halmaahauri,
Tumeanzisha mradi mpya wa majaribio wa kuratibu makazi tutaanza katika wilaya mbili za Kinondoni na Ubungo,” amesema.

Aidha, Lukuvi amewataka wananchi wenye kero za ardhi kutoa malalamiko yao ili wizara iyafanyie kazi.

Na Regina Mkonde

Share:

Leave a reply