Waziri Mkuu Majaliwa afungua maonyesho ya 12 elimu vyuo vikuu

978
0
Share:

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa leo Julai 26, 2017 jijini Dar es Salaam, amefungua maonyesho ya kumi na mbili ya Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia yaliyoandaliwa na Tume ya Vyuo Vikuu nchini (TCU) ambapo takribani Taasisi za elimu ya juu 80 kutoka ndani na nje ya nchi, zinashiriki maonyesho hayo. 

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa maonyesho hayo yanayofanyika kwenye viwanja vya Mnazi Mmoja, Majaliwa amezitaka taasisi hizo kuandaa mikakati ya kupunguza tatizo la ajira kwa kutoa mafunzo kwa wanafunzi yanayoendana na soko la ajira na fursa zilizopo.

“Tatizo la ajira limekuwa likiongezeka, lakini serikali inaendelea kutatua tatizo hilo. Taasisi zote zinazosimamia elimu ya juu zihakikishe vyuo vikuu vinatoa programu zinazowezesha mwanafunzi kujiajiri, pia programu zinazokidhi mahitaji ya kiuchumi hasa katika sekta ya viwanda, mafuta, gesi na madini ambapo wataalamu wake ni wachache hapa nchini,” amesema.

Aidha, Majaliwa amesema serikali itaendelea kutenga bajeti ya kutosha kwenye sekta ya elimu ili kuongeza fursa ya wanafunzi kusoma bure, kukarabati miundombinu ya shule za serikali kongwe, kutoa vifaa vya kutosha vya kufundishia wanafunzi hasa wa masomo wa sayansi pamoja na fedha za utafiti wa maendeleo kwa ajili ya kuimarisha ubunifu na teknolojia.

Naye Waziri wa Viwanda na Uwekezaji, Charles Mwijage amezitaka taasisi hizo kutoa wataalamu watakaoschochea uchumi wa viwanda kwa ajili ya kuleta maendeleo ya nchi. 

“Serikali inatarajia kuzindua mpango wa pili wa miaka 5 wenye dhima ya kujenga uchumi wa viwanda na kuleta maendeleo ya watu,na nyie ndio wadau wakuu wa maendeleo hayo,” amesema.

Na Regina Mkonde

Share:

Leave a reply