Waziri Ummy aibeba timu ya African Sports ya Tanga, aikabidhi mil. 2.1

200
0
Share:

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mhe. Ummy Mwalimu ameikabidhi msaada wa fedha Tsh. 2,100,000 klabu ya African Sports ya mkoani Tanga ambao utatumika kulipa posho za wachezaji wa timu hiyo inayoshiriki Ligi daraja la Pili Tanzania Bara.

Akikabidhi msaada huo, Waziri Ummy ambaye pia ni Mbunge Viti Maalum Mkoa wa Tanga alisema amedhamiria kusaidia timu hiyo na kuhakikisha inashiriki Ligi Kuu ya Tanzania Bara jambo ambalo litasaidia kuongeza fursa mbalimbali za kiuchumi na kijamii katika jiji la Tanga.

“Michezo ni ajira, michezo ni afya, michezo ni burudani, tumeanza safari kuitoa African Sports Club ya Tanga kwenye Ligi Daraja la Pili hadi Ligi Kuu 2019/2020,” alisema Waziri Ummy wakati akikabidhi msaada huo kwa uongozi wa klabu ya African Sports.

Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto na Mbunge Viti Maalum Mkoa wa Tanga, Mhe. Ummy Mwalimu akizungumza na viongozi na wachezaji wa timu ya African Sports baada ya kukabidhi msaada wa milioni 2.1

Pamoja na kukabidhi msaada huo pia Mhe. Ummy amewafungulia akaunti za benki wachezaji wote wa African Sports katika Benki ya NMB ili iwe rahisi posho zao kulipwa moja kwa moja kupitia benki ili kuepusha migogoro lakini pia kulipia Tsh. 500,000 ya leseni za wachezaji na ada ya ushiriki wa timu kwa Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF).

Aidha Waziri Ummy alisema kampuni ya mafuta ya GBP mkoani Tanga imeichangia klabu hiyo milioni tatu na kuwataka wachezaji kucheza kwa bidii ili kuisaidia timu hiyo kupata mafanikio makubwa.

“Nao wanaiunga mkono African Sports. Tunataka ushindi, msituangushe.” Waziri Ummy aliwaambia wachezaji wa African Sports.

Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto na Mbunge Viti Maalum Mkoa wa Tanga, Mhe. Ummy Mwalimu akifurahi na viongozi na wachezaji wa timu ya African Sports baada ya kukabidhi msaada wa milioni 2.1 Mwenyekiti wa Wazee wa timu ya African Sports akitoa neno la shukrani kwa Waziri Ummy baada ya kuwakabidhi msaada wa milioni 2.1 ambazo zitatumika kulipa posho kwa wachezaji wa timu hiyo.

Share:

Leave a reply