Waziri Ummy asisitiza usawa wa kijinsia katika elimu

489
0
Share:
Wazazi na walezi wametakiwa kutoa kipaumbele cha elimu kwa watoto wakike kutokana na Serikali kutoa fursa ya elimu bure kwa shule za Msingi na Sekondari ili kuongeza usawa wa kijinsia katika elimu.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu wakati akifungua Kongomano la kwanza la Kimataifa la Kijinsia lililoandaliwa na Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Dar es Salaam (DUCE) ambapo alimwakilisha Makamu wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan leo Jijini Dar es Saalam.
Waziri Ummy alisema kuwa uamuzi wa Serikali ya Awamu ya Tano kutoa elimu bure  unatoa fursa zaidi kwa mtoto wa kike kunufaika na elimu tofauti na awali ambapo kutokana na hali ya maisha kuwa duni familia nyingi  zilitoa kipaumbele kwa mtoto wa kiume na
kuwaacha wakike kufanya shughuli za nyumbani.
“Niwaombe wataalam wetu tuungane kwa pamoja kuhakikisha watoto wa kike wanapewa fursa sawa katika kujiunga na masomo, ata waliopata mimba kwa bahati mbaya wapewe fursa ya kurudi mashuleni,” alisema Waziri Ummy.
Aidha aliongeza kuwa ili kuleta asilimia hamsini kwa hamsini kwa wote wazazi wanatakiwa kuwahamasisha watoto wakike kupenda masomo ya Sayansi kwani inaonesha watoto wengi wakike hawana hamasa na masomo hayo.
Aidha aliupongeza uongozi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kwa kuweza kufanikisha kuwa na wanafunzi wakike asilimia 38 wakati Serikali imefanikisha asilimia 32 ya wanafunzi wakike katika elimu ya juu.
Kwa upande wake Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Profesa Rwekaza Mukandala alisema kuwa tangia mwaka 1993
kulikuwa na mikakati ya kuwaweka watoto wa kike katika fani mbalimbali na kuwapa ujuzi ambapo imeonesha watoto wengi wa kike walikuwa wanaongoza kwa kufanya vizuri zaidi.
Nae Mkuu wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Dar es Salaam (DUCE) Profesa William Anganisya alisema kuwa Kongamano hilo litaonesha nafasi ya mwanamke katika jamii na kuwa chachu kwa watoto wakike kupenda masomo ya Sayansi.
Serikali imejipanga kuja na mikakati mipya madhubuti ya kuboresha idadi ya wanafunzi wa kike hasa katika elimu ya juu ili
kuleta usawa wa kijinsia.

Share:

Leave a reply