Waziri Ummy azindua utafiti wa kitaifa unaohusu sababu na athari za ndoa za utotoni

462
0
Share:

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu amefanya uzinduzi wa utafiti wa kitaifa kuhusu sababu na athari za ndoa za utotoni, utafiti ambao umefanywa na taasisi ya Repoa katika mikoa mbalimbali nchini kati ya mwaka 2015 na 2016.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Waziri Ummy amesema serikali inatambua fika kuwepo na idadi kubwa ya wasichana ambao wamekuwa wakiolewa na kupewa mimba kabla ya kufikisha miaka 18 na ila serikali ina mikakati mbalimbali ya kuhakikisha vitendo hivyo vinamalizika.

Ummy alisema kikwazo kikubwa kwa sasa ni Sheria ya Ndoa ya 1971 na kupitia wizara yake amekuwa akifanya jitihada mbalimbali ili ibadilishwe lakini wakati juhudi zikifanyika ili ifanyiwe marekebisho wanaweza kutumia Sheria ya Elimu ya 2016 ambayo inasema mtu yoyote atakayempa mwanafunzi mimba atafungwa kifungo cha miaka 30.

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu.

“Sheria ya Ndoa ya mwaka 1971 inawaumiza sana watoto wa kike na ndiyo kichocheo kikubwa cha ndoa na mimba za utotoni na watu wengi wamekuwa wakidhani jambo hili lipo chini yangu lakini ni tofauti, sheria hii ipo pia Wizara ya Katiba na Sheria na nimekuwa nikifanya mazungumzo na waziri ili ifanyiwe marekebisho,

“Mimi nia yangu ni Sheria ya Ndoa ibadilishwe, umaskini hauwezi kuondolewa kwa kwa kuozesha watoto wa kike lakini pia taasisi ziwezinakwenda vijijini huko ndiyo watu wengi hawana elimu kuhusu haya mambo na mabinti pia wanatakiwa waelimishwe ili wajue haki zao za kimsingi,” alisema Waziri  Ummy.

Nae Msaidizi wa Mwakilishi wa Shirika la Idadi ya Watu UNFPA, Christine Mwanukuzi alisema utafiti huo ni mzuri kama utafanyiwa kazi na serikali na mashirika ili kuwasaidia watoto wa kike kwani umeonyesha jinsi hali ilivyo kwa sasa nchini na hatua ambazo zinaweza kuchukuliwa ili kumaliza tatizo hilo katika jamii ya Tanzania.

Msaidizi wa Mwakilishi wa Shirika la Idadi ya Watu UNFPA, Christine Mwanukuzi.

“Utafiti wa mwaka 2010 wa kigeografia na afya ulionyesha kuna mikoa tatizo ni kubwa na hivyo basi tunategemea utafiti wa sasa utatupa picha ya hali halisi ilivyo nchini na utumike kama chachu ya kuleta msukumu kuongeza juhudi za kumaliza vitendo hivi,

“Ni vyema utafiti huu utumike kufanya marekebisho kama kubadili sheria na sera ambazo zinawakandamiza watoto wa kike lakini pia mapendekezo ambayo yametolewa na watafiti yafanyiwe kazi,” alisema Mwanukuzi.

Nae Mtaalamu wa masuala ya uchumi kutoka Taasisi ya Utafiti wa Kupunguza Umaskini (Repoa), Dk. Lucas Katera alisema katika utafiti huo wamebaini kuwa sababu kubwa ya watoto wa kike kuolewa na hata kusababisha ndoa za utotoni ni mila na desturi, michezo ya unyago, umaskini, mwonekano wa wasichana lakini pia jamii kukosa elimu kuhusu mambo hayo.

Mtaalamu wa masuala ya uchumi kutoka Taasisi ya Utafiti wa Kupunguza Umaskini (Repoa), Dk. Lucas Katera.

Dk. Katera alisema hatua ambazo zinaweza kuchukuliwa ni pamoja na jamii ihusishwe ili ijue jinsi hali ilivyo nchini na madhara ya vitendo hivyo, kuwepo namba ya simu ambayo watu watakuwa wakitoa taarifa na kesi ambazo zinahusu ndoa na mimba za utotoni zitolewe maamuzi haraka.

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu akizindua utafiti wa kitaifa kuhusu sababu na athari za ndoa za utotoni.

Share:

Leave a reply