Waziri Ummy Mwalimu azitaka Halmashauri kutoa vitambulisho kwa Wazee

161
0
Share:

Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mhe Ummy Mwalimu (Mb.) amezitaka Halmashauri zote nchini kutoa vitambulisho kwa wazee waliopo katika Halmashauri zao. Haya ameyasema leo wakati akifungua Mkutano Mkuu wa mwaka wa Mtandao wa Mashirika ya Wazee, uliofanyika Mkoani Dodoma katika Ukumbi wa Maktaba Kuu ya Mkoa.

Akihutubia katika uzinduzi wa Mkutano huo Mheshimiwa Waziri Ummy alizitaka Halmashauri kuhakikisha wanatekeleza wajibu wao wa kutoa vitambulisho kwa wazee ili kuwezesha utambuzi wa wazee waliopo katika Halmashauri zao hususan katika utoaji huduma na mahitaji mbalimbali.

Waziri Ummy alisisitiza kuwa Halmashauri zinatakiwa kutekeleza kwa vitendo kaulimbiu ya “Mzee Kwanza” hususan katika utoaji wa huduma za afya ambapo kila kituo cha Afya cha Umma kinatakiwa kiwe na chumba na watumishi maalum wa kuhudumia wazee. Pia ameziagiza Halmashauri zote nchini kuhakikisha wanakuwa na regista ya Wazee kwa kuainisha pia ujuzi wa wazee hao.

Mheshimiwa Waziri Ummy alieleza kuwa Serikali inatarajia kuwasilisha muswada wa sheria ya Wazee Bungeni Mwezi Septemba mwaka huu. Pia, aliwahakikishia wazee kuwa tatizo la upatikanaji wa dawa kwa wazee litapatiwa ufumbuzi kwa kiasi kikubwa kuanzia mwezi Julai 2016.

 

Share:

Leave a reply