Wizara ya Afya Zanzibar yapokea msaada wa dawa na vifaa tiba kutoka Serikali ya watu wa China

402
0
Share:

Mkurugenzi  Bohari Kuu ya Dawa Zanzibar  Zahran Ali Hamad amesema upatikanaji wa huduma ya dawa muhimu katika wodi za wazazi umefikia asilimia 96 na wazazi wamekuwa wakipata huduma bila usumbufu.

Amesema Bohari Kuu ya dawa hivi sasa imeimarika na wamekuwa wakisambaza dawa hizo katika Hospitali na vituo vya Afya kwa wakati kwa mujibu ya mahitaji yao.

Mkurugenzi Zahrani ameeleza hayo Ofisini kwake  Maruhubi baada ya Wizara ya Afya kupokea msaada wa dawa na vifaa tiba venye thamini ya zaidi ya shilingi milioni 420 kutoka Serikali ya  Watu wa China.

Amesema kuimarika kwa huduma ya dawa na vifaa tiba, ni juhudi zinazochukuliwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na wafadhili wengine wa maendeleo katika kuwapunguzia wananchi umasikini.

“Bohari Kuu hivi sasa imejaa dawa na tumeboresha sana huduma katika wodi za wazazi hasa Hospitali Kuu ya Mnazimmoja,” alisisitiza Ndugu Zahrani.

Hata hivyo Mkurugenzi wa Bohari Kuu ya dawa alisema wamekuwa wakifuatilia kwa karibu mazingira ya kuzihifadhi dawa hizo katika vituo vya Afya na kuhakikisha zinawafikia walengwa.

Alisema msaada uliotolewa na Serikali ya China, ikiwa ni mara ya pili katika kipindi kisichozidi miezi mitatu, sehemu kubwa ni kwa ajili ya wagonjwa wa maradhi ya kuambukiza, sindikizo la damu na sukari ambapo hulazimika kuzitumia kwa muda mrefu na bei zake ni ghali.

Akimkabidhi Waziri wa Afya msaada huo, Balozi mdogo wa China aliepo Zanzibar Xie Xiaowu alisema nchi yake itaendeleza mashirikiano ya kihistoria yaliyoanzishwa na waasisi wa nchi mbili hizi Abeid Amani Karume na Maotse Tung kwa faida ya wananchi wake.

Ameahidi kuendelea kutoa mashirikiano zaidi katika uchumi wa Zanzibar kwa kuimarisha miundo mbinu na kusaidia vifaa tiba na dawa za aina mbali mbali.

Nae Waziri wa Afya Mahmoud Thabit Kombo aliishukuru China kwa misaada inayotoa kwa Zanzibar na hasa sekta ya afya ambayo imesaidia kuboresha upatikanaji wa huduma katika Hospitali na vituo vya afya.

Ramadhani Ali/Maelezo Zanzibar

Waziri wa Afya Zanzibar Mahmoud Thabit Kombo na Balozi mdogo wa China aliepo Zanzibar  Xie Xiaowu wakisaini hati ya makabidhiano ya dawa zilizotolewa Serikali ya watu wa China

Wafanyakazi wa Bohari Kuu ya Dawa Zanzibar na wanafunzi wa fani ya ufamasia wakifuatilia sherehe ya kukabidhiwa dawa zilizofanyika Bohari Kuu ya Maruhubi.

Mkurugenzi wa Bohari Kuu ya Dawa Zanzibar Zahran Ali Hamadi akizungumza na wandishi wa habari (hawapo pichani) kuhusu kubore kwa hali ya dawa Zanzibar baada ya Waziri wa Afya Zanzibar kukabidhiwa msaada wa dawa kutoka Serikali ya watu wa China.

Balozi mdogo wa China aliepo Zanzibar Xie Xiaowu akimkabidhi Waziri wa Afya Zanzibar Mahmoud Thabit Kombo msaada wa dawa uliotolewa na Serikali ya China makabidhiano haya yamefanyika Bohari Kuu ya dawa Maruhubi Mjini Zanzibar.

Picha na Makame Mshenga-Maelezo.

 

 

Share:

Leave a reply