Kutoka Bungeni: Wizara ya Ardhi kubaini taasisi zinazodaiwa fidia na wananchi

261
0
Share:

Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi katika  kipindi cha mwaka wa fedha 2016/2017 itabaini taasisi zote na watu binafsi wanaodaiwa fidia na wananchi ili waweze kulipa fidia hizo.

Akiongea leo Bungeni, mjini Dodoma Naibu Waziri wa Wizara hiyo Mhe. Angelina Mabula amesema kuwa ni kweli tatizo hilo lipo na tayari Serikali imechukua hatua kwa kuzielekeza Halmashauri zote na taasisi nyingine kulipa fidia stahiki kwa wananchi pale wanapotaka kutwaa maeneo yao.

Mhe. Mabula amesema kuwa taasisi nyingi zimekuwa zikichukua mashamba ya wananchi na kushindwa kuwalipa fidia hivyo kulimbikiza madeni hayo kwa muda mrefu hali inayokwamisha shughuli  za maendeleo.

“Halmashauri za Wilaya, Taasisi na Maafisa Ardhi hawaruhusiwi kuchukua mashamba ya wananchi kabla hawajakamilisha utaratibu wa malipo ya fidia kwa wananchi hao, ili kuondokana na malimbikizo ya madeni ya fidia ambayo malipo yake huchukua muda mrefu na kurudisha nyuma maendeleo ya wananchi,” alisema Mhe. Mabula.

Aidha Mhe. Mabula amewataka wananchi wanaodai fidia kuwa wavumilivu wakati Wizara yake inaendelea kufanya upembuzi wa taasisi hizo ili ziweze kulipa fidia zote zinazodaiwa na wananchi.

Vilevile Wizara hiyo imetoa ramani za mitaa kwa wenyeviti wa mitaa wa Jiji la Dar es Salaam ili wenyeviti hao waweze kutambua matumizi ya maeneo yao, kwa mfano maeneo ya wazi, na nini kijengwe katika maeneo yao kama vile nyumba fupi au ndefu, hoteli au chuo ili kuondokana na migogoro ya kubolewa nyumba kwa kujenga eneo lisiloruhusiwa.

“Tumeanza kwa mkoa wa Dar es Salaam lakini zoezi litaendelea kila Mkoa na kila Wilaya Nchi nzima, ili Wenyeviti wa Mitaa na Vijiji waweze kutambua matumizi ya maeneo yao, hivyo kuchukua hatua kwa haraka pindi ambapo maeneo hayo yanatumika tofauti na matumizi yaliyoko” alifafanua Mhe. Mabula.

Aidha Mhe. Mabula amezitaka Halmashauri kwa kushirikiana na Wizara ya Ardhi, Nyumba, na Maendeleo ya Makazi kuwapa uwezo wenyeviti hao ili waweze kufanya kazi hiyo kiufanisi.

Magari yanayoingizwa nchini kwa msamaha wa kodi kuwa na namba na rangi maalum

Katika kuthibiti matumizi  ya magari yanayoingia Nchini kwa msamaha wa kodi  Serikali imesema kuanzia Julai Mosi magari hayo sasa yatakuwa na namba na rangi maalum.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Mpango alipokuwa akiongea na waandishi wa habari mjini Dodoma kuhusu tamko la kuondoa misamaha ya kodi kwenye taasisi za dini kwa kuwa zinatoa huduma za kijamii kama shule na hospitali.

“Kwa kutambuua mchango mkubwa wa Taasisi mbalimbali za kidini katika utoaji wa huduma za elimu na afya, napendekeza kufuta utaratibu niliotangaza katika hotuba ya bajeti na badala yake Serikali itaimarisha zaidi hatua mbalimbali za uthibiti misamaha ya kodi ikiwemo magari yaliyoingia kwa msamaha wa kodi kuwa na namba na rangi maalum,” alifafanua Mhe.Dkt. Mpango.

Aliendelea kutaja hatua nyingine kuwa ni taasisi za kidini kuwasilisha vifaa vinavyotarajiwa kununuliwa kutoka nje ya nchi kila mwazo mwa mwaka wa kalenda na kuthibitisha kama vifaa vilivyopewa msamaha mwaka uliopita vilitumika kama sheria inavyotaka.

Pia, kuwasilisha majina ya watu walioidhinishwa na Shirika au Taasisi kuandika barua ya kuomba msamaha wa kodi, wakiainisha cheo, saini, picha, anwani na namba zao za simu ili kuiwezesha Mamlaka ya Mapato Tanzania kufuatilia bidhaa zilizoombewa na kupewa msamaha kama zimepata kibali cha taasisi hizo.

Vile vile taasisi hizo zinatakiwa kupata barua kutoka kwa Afisa Mtendaji wa Serikali ya Mtaa na Mkuu wa Wilaya mahali Taasisi au Mradi unaotekelezwa ulipo.

Mhe. Mpango amesema kuwa hatua hizo zimekuja kutokana na bidhaa zinazoombewa msamaha wa kodi kutumika tofauti na kusudi la msamaha huo.

Aidha ametoa tahadhari kwa mashirika ya kidini kuanzia sasa, kuhakikisha kuwa yanafuata taratibu zote na Kuzingatia masharti ya msamaha unaotolewa ili kuepuka kufutiwa leseni zao pale zitakapokwenda kinyume na sheria na kanuni zilizowekwa.

2Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI Mhe. George Simbachawene akitoa maelezo wakati wa kipindi cha maswali na majibu Bungeni leo ambapo alieleza kuhusu hatua  zinazochukuliwa na Serikali katika kuimarisha huduma za afya katika Halmashauri zote nchini kwa kujenga Vituo vya Afya na Zahanati ili kuimarisha huduma hizo.

7Sehemu ya Watoto kutoka Kituo cha Shirika na  Malezi Endelevu (SHIME) cha mjini Dodoma wakiwa ndani ya ukumbi wa Bunge kujionea namna Bunge linavyotekeleza majukumu yake

8Mbunge wa Jimbo la Mtwara Vijijini Mhe. Hawa Ghasia akisisitiza jambo kwa Waziri wa Habari Utamaduni  Sanaa na Michezo Mhe. Nape Nnauye leo Bungeni Mjini Dodoma.

unnamedNaibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Tulia Ackson Akitoka nje ya ukumbi wa Bunge leo mara baada ya kuahirisha shughuli za Bunge Mjini Dodoma.

Share:

Leave a reply