Wizara ya madini kwachafuka, makinikia kumng’oa Prof. Muhongo

1037
0
Share:

Rais John Magufuli amemtaka Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo kuachia madaraka, pia amemsimamisha kazi mkurugenzi mtendaji wa Wakala wa Ukaguzi wa madini (TMAA) pamoja na kuivunja bodi ya wakala huo.

Licha ya hayo, Rais Magufuli ameviagiza vyombo vya dola ikiwemo Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kuanza kuwachunguza wafanyakazi wa Wizara ya Nishati na Madini walio katika sekta ya madini pamoja na wale wa TMAA na kuwachukulia hatua za kisheria. Hali kadhalika amevitaka vyombo vya ulinzi na usalama kuhusika katika shughuli zote za madini ili kuhakikisha madini hayatoroshwi ovyo nje ya nchi. 

Rais Magufuli amechukua hatua hiyo leo Mei 24, 2017 Ikulu jijini Dar es Salaam baada ya kupokea taarifa ya Kamati Maalumu ya wataalamu wa uchunguzi wa mchanga wenye madini (makinikia) ulio katika makontena 277 yaliyozuiliwa kusafirishwa nje ya nchi miezi kadhaa iliyopita kutokana na kuwepo kwa utata wa  viwango vya madini yaliyoko kwenye makontena, sambamba na mikataba yake kutokuwa wazi, hali iliyoleta hofu kuwa nchi inaibiwa kupitia makinikia.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo iliyotolewa na Mwenyekiti wa kamati, Profesa  AbdulKarimu Mrumba, imebaini viwango vya juu vya madini yaliyoko ndani ya makinikia tofauti na taarifa ya awali iliyotolewa na TMAA na kwamba tofauti hiyo inaonyesha upotevu wa mapato ya serikali kupitia zoezi la ukokotoaji mirabaha inayolipwa serikalini.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akipokea Taarifa ya uchunguzi wa mchanga wa madini mbalimbali uliotakiwa kusafirishwa nje ya nchi kutoka kwenye machimbo ya madini nchini kutoka kwa Mwenyekiti wa Kamati hiyo Profesa Abdulkarim Hamis Mruma Ikulu jijini Dar es Salaam.

Ambapo kwa upande wa madini ya dhahabu pekee, taarifa hiyo ya uchunguzi inaonyesha serikali ilitakiwa kupata mrabaha wa bilioni 676 wakati TMAA inaonyesha mrabaha wa serikali ni bilioni 97.Na kwa hivyo, jumla ya thamani ya madini yote ya makimikia yaliyoko kwenye makontena 277 ni bilioni 829.4 kwa kutumia viwango vya wastani na ni trilioni 1.439 kwa kutumia viwango vya juu.

Aidha, ripoti hiyo imebaini kuwa kuna madini ya mkakati yenye thamani inayofanana na dhahabu ambayo kwa sasa yana soko kubwa duniani, yenye jumla ya thamani ya bilioni 126.5 hadi 261.5 yaliyoko katika makontena 277, ambayo hayakuorodheshwa katika makinikia hayo pamoja na kutotumika katika ukokotoaji mrabaha na kuisababishia serikali upotevu wa mapato.

Kufuatia udanganyifu huo ulioisababishia serikali upotevu wa mapato, Rais Magufuli amesema kulikuwa na makusudi yaliyofanywa na baadhi ya viongozi wa wizara husika kwa kutochukua juhudi za kununua mashine za kuchenjua madini (smelter) kwa masilahi yao binafsi, pamoja na kwamba sera ya madini ya 2009 inaagiza wizara kufanya juhudi za kuwa na smelter hapa nchini.

“Ripoti hii haiwezi kupita hivi hivi, ikipita hivi hivi tutakuwa watu wa ajabu tunahitajika kufanya kitu, wakati tukisubiri ripoti nyingine, mapendekezo yote ya kamati tumeyakubali, Bodi ya TMAA nimeivunja kuanzia leo, mkurugenzi mtendaji wa TMAA anasimama kazi, vyombo vya dola na takukuru muanze kufuatilia wafanyakazi wa TMAA waliohusika na yote, hatua za kisheria zianze kuchukuliwa kuanzia leo,” amesema na kuongeza.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akizungumza mara baada ya kupokea ripoti hiyo ya uchunguzi wa mchanga wa madini uliotakiwa kusafirishwa nje ya nchi kutoka kwenye machimbo mbalimbali ya madini nchini.

“Katika shughuli zote zinazofanyika katika nchi zinazohusu madini vyombo vya ulinzi na usalama vianze kutumika, muunde tume au group kuhakikisha mali zetu zote zinazohusiana na madini hazitoroshwi ovyo, madini yetu yanaishia kwenye nchi Fulani ni mengi mno. Lakini wizara wameshindwa kusimamaia TMAA, imeshindwa kusimamia ujenzi wa smelter, kuweka utaratibu wa kufuatilia makemikia,

“Kamishana wa madini anafanya nini? Waziri anafanya nini? Na kwa sababu hiyo vyombo viwachunguze baadhi ya watendaji wa wizara ya madini waliokuwa wanahusika na sekta ya madini, Lakini kwa haya yote, ninampenda sana profesha muhongo na ni rafiki yangu, lakini kwenye hili ajifirikie, na bila kuchelewa nilitaka aachie madaraka.”    

Dkt. Magufuli amesema kwa sasa nchi iko katika vita ya uchumi, na kwamba ana majina ya watu waliotaka kuingilia na kuharibu uchunguzi wa madini hayo ili kupoteza ushahidi. Huku akieleza kuwa, kwenye ripoti hiyo hakuna sehemu inayoonyesha panakopelekwa makinikia ya nchi kwa ajili ya uchenjuaji.

Aidha, Kamati hiyo iliyowasilisha ripoti yake leo, iliagizwa kubaini aina, kiasi, viwango vya ubora na thamani ya madini yaliyomo katika makontena hayo ambayo yalikuwa katika utaratibu wa mwisho wa kusafirishwa kwenda nje ya nchi kwa ajili ya kwenda kuchenjuliwa madini yaliyomo ndani yake.

Na Regina Mkonde

Share:

Leave a reply