Yaliyojiri kwenye soko la hisa wiki iliyoisha Ijumaa tarehe 14 Julai 2017

354
0
Share:

Meneja Masoko Mwandamizi wa Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE), Marry Kinabo amesema thamani ya mauzo ya hisa kwa wiki hii imepungua kwa 36% kutoka Sh. bilioni 6 wiki iliyopita hadi bilioni 3.9 wiki hii iliyoishia tarehe 14 Julai 2017.

Kinabo ameyaeleza hayo leo Julai 17,2017 wakati akizungumza na wanahabari.Hata hivyo amesema idadi ya hisa zilizouzwa na kununuliwa katika soko hilo imepanda kwa 26% kutoka hisa 13.6 hadi hisa milioni 17 kwa wiki iliyoishia 14 Julai 2017.

Kwa upande wa mauzo ya hati fungani amesema “Tofauti na ilivyokuwa kwenye hisa, mauzo ya hati fungani katika wiki iliyoishia tarehe 14 Julai 2017 yamepanda kutoka bilioni 12.25 wiki iliyopita hadi Shilingi Bilioni 44.3. Mauzo haya yalitokana na hatifungani kumi na saba (17) za serikali na za Makampuni binafsi (Corporate Bonds) zenye jumla ya thamani ya Shilingi bilioni 51 kwa jumla ya gharama ya Shilingi Bilioni 44.3.”

Kuhusu ukubwa wa mtaji wa kampuni zilizoorodheshwa katika soko, amesema umepanda kwa Bilioni 516 kutoka Shilingi Trilioni 18.7 wiki iliyopita hadi Trilioni 19.2 wiki iliyoishia tarehe 14 Julai 2017. Kutokana na kupanda kwa bei za hisa za USL (34%), ACA (9%) na JHL (5%).

“Ukubwa wa mtaji wa kampuni za ndani umepanda kwa Shilingi Bilioni 13.5 kutoka Shilingi Trilioni 7.70 wiki iliyopita hadi Shilingi Trilioni 7.72 wiki hii. Hii ni kutokana na kupanda kwa bei ya hisa za CRDB (2.5%),” amesema.

Aidha, amesema Kiashiria cha kampuni zilizoorodheshwa katika soko yaani DSEI kimepanda kwa pointi 59 kutoka pointi 2,151 hadi pointi 2,211 kutokana na kuongezeka kwa bei za hisa za kampuni mbali mbali zilizopo sokoni. Pia Kiashiria cha Sekta ya huduma za kibiashara (CS) wiki hii imebaki kwenye wastani wa 2,467 kama awali.

“Kufuatia kupanda kwa bei za hisa, kishiria cha kampuni za ndani yaani TSI kimepanda kwa pointi 6 kutoka pointi 3,666 wiki iliyopita hadi pointi 3673 wiki hii, wakati Kiashiria cha sekta ya viwanda (IA) imebaki kama awali kwenye wastani wa TZS 4809 huku Kiasharia cha huduma za kibenki na kifedha (BI) wiki hii kimepanda kwa pointi 17 kutoka pointi 2,598 hadi pointi 2,616 kutokana na ongezeko la bei ya hisa za CRDB (2.5%),” amesema.

Na Regina Mkonde

Share:

Leave a reply