Zahanati ya Kanisa la EAGT Singida yatoa msaada kwa makundi yasiyojiweza

447
0
Share:

Zahanati ya Utemini mjini hapa inayomilikiwa na kanisa la Evangelistic Assembles of God Tanzania (E.A.G.T.),imetoa msaada wa tani 100 za mchele, unga, maharage, dagaa na sukari kwa wazee, walemavu na makundi yasiyojiweza. Msaada huo una thamani ya zaidi ya shilingi 5.2 milioni.

Msaada huo ambao utakuwa endelevu na utakuwa ukitolewa na shirika la Global Education Development Fund (GEDF) la nchini Canada na zahanati ya Utemini ikasimamia.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake, Mkurugenzi wa zahanati hiyo, Askofu John Joseph Mafwimbo, alisema msaada huo unatarajiwa kunufaisha zaidi ya walengwa elfu moja.

“Kwa siku ya leo (juzi) tumewasaidia wazee, walemavu na watu wasio jiweza 670 na kila moja amepata mchele kilo tatu, unga, maharage, dagaa na mafuta ya kulai,” alisema Askofu Mafwimbo.

Alisema msaada huo utakuwa endelevu, kwa lengo la kuwapunguzia makali ya maisha walengwa hao.

Aidha, Mkurungezi huyo ambaye pia ni askofu wa E.A.G.T mkoani Singida na askofu msaidizi wa kanda ya kati, amesema msaada huo unakabiliwa na changamoto kubwa ya kuingiliwa na watu wengi wasiokuwa na sifa.

“Anakuja mtu ukimwangilia unashangaa ni kwa nini anafuata msaada wakati hana kilema wala sio mzee, ana nguvu za kutosha kumwezesha kufanya kazi akajipatia riziki. Kuna mmoja nilimuuliza mbona wewe huna sifa ya kunufaika na msaada huu, akaniambia ametorokwa na mume, hivyo hana uwezo wa kujipatia chakula,” alisema.

Amesema wamejipanga vizuri kuhakikisha ni walengwa tu, ndio watapata chakula. Walemavu watakuwa wanapelekewa msaada wa chakula majumbani kwao.

Kwa mujubu wa Mkurugenzi Mafwimbo, Shirika hilo la GEDF linatarajia kuanzisha mradi wa ujenzi wa vyoo katika shule za Manispaa ya Singida na kutoa chakula cha mchana. Pia wataanzisha kituo kwa ajili ya watu watakaohitaji supu.

Na Nathaniel Limu, Singida

Share:

Leave a reply