Zaidi ya watoto 25,000 kupata kansa kila mwaka

461
0
Share:

Katika Kuadhimisha Siku ya Saratani duniani, Mkurugenzi wa Mambo ya Nje wa Asasi ya Marafiki wa Watoto wenye Saratani Tanzania (FoCC), Janeth Manoni amesema kwa sasa ugonjwa huo umekuwa tishio kwa watoto nchini, ambapo inakadiriwa zaidi ya watoto 25,000 hupata ugonjwa huo kila mwaka.

Manoni ameyasema hayo, jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari ambapo amesema kuwa watoto wengi hufariki dunia baada ya  kuchelewa kupata matibabu kufuatia jamii kutojua dalili za awali za ugonjwa huo.

“Saratani ya watoto imekua janga hususan kwamba wengi hupoteza maisha kufuatia jamii kutotambua dalili za awali za ugonjwa huo ambapo uhusisha na magonjwa ya kishirikina kitendo kinachopelekea kuchelewa kupata matibabu na kufariki dunia. Kuna umuhimu kwa watu wa afya, wazazi na walezi kuzijua dalili hizo,” amesema.

“Jamii ielewe kuwa saratani ipo na zaidi kwa watoto, wengi hucheleweshwa hospitalini sababu ya dalili zake za awali kutofahamika na hufanana na dalili za magonjwa mengi lakini kuna uhakika wa asilimia 85 wa watoto hao kupona wanapowahishwa hospitali,” amesema.

Manoni amesema asasi yake itaadhimisha siku ya saratani Jumamosi ya Februari 18,2017 katika viwanja vya DonBosco ambapo kutatolewa huduma za uchunguzi wa saratani kwa watoto bure, na kuwataka wazazi na walezi kuwapeleka watoto wao kufanyiwa uchunguzi.

Mhamasishaji wa FoCC, Remigius Kazaura amesema ongezeko la ugonjwa wa saratani kwa watoto linatokana na mabadiliko ya mfumo wa maisha hasa ulaji wa vyakula visivyo vya asili.

“Mfumo huu tunaoishi ndio sababu ya ongezeko la ugonjwa huo, ikiwemo ulaji wa vyakula visivyo vya asili hasa vinavyopakiwa kwenye makopo au mifuko ya plastiki, hakika plastiki imetawala maisha yetu ambapo athari zake zinasabaisha saratani,” amesema.

Share:

Leave a reply